Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mjini Mhe. Juma Rahibu akimkabidhi funguo na Kadi ya Bajaji mpya Kijana Lyanga Kitundu wakati akizindua huduma za Mikopo ya Bajaji kwa Vijana kutoka Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL), (katikati) Mrajis Msaidizi wa Mkoa wa Kilimanjaro Jaquline Senzige akifuatiwa na Meneja Mkuu wa KCBL Godfrey Ngura (kulia),Katibu wa Waendesha Bajaji (kushoto) Rashid Omari wakati wa makabidhiano yaliyofanyika hivi karibuni Viwanja vya Manyema Mkoani Kilimanjaro

Meneja Mkuu wa Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) Godfrey Ngura akieleza mikakati ya Benki hiyo katika kupanua wigo wa utoaji huduma kwa wananchi wengi ili waweze kufikiwa na huduma za kifedha wakati wa uzinduzi wa bidhaa ya mikopo ya Bajaji kwa Vijana Mkoani Kilimanjaro


Bajaji zilizozinduliwa

.......................................................................

Na Mwandishi Wetu

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi Mjini Mhe. Juma Rahibu ameipongeza Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) kwa hatua ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza fursa za ajira kwa vijana kupitia bidhaa mpyaya Benki hiyo ya mikopo ya Bajaji kwa Mkoani Kilimanjaro.

Mhe. Juma Rahibu amesema hayo wakati wa akizindua rasmi bidhaa ya huduma ya mikopo ya Bajaji kwa vijana katika Viwanja vya Soko la Manyema Manispaa ya Moshi Mjini Desemba 15,2021

Mstahiki Meya ameishukuru Benki ya KCBL kwa hatua hiyo kwani kwa kubuni na kuanzisha mikopo hiyo kutaongeza kasi ya Maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla kwa kuwawezesha wananchi kupunguza umaskini na kuongeza uwezo wa kujitegemea wenyewe. Jambo ambalo amesisitiza kuwa litasaidia Serikali katika kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kujikwamua na kuiomba Benki hiyo kuendeleza jitihada hizo kwa makundi mengine maalum ya Wanawake na Walemavu.

“Niwaombe sana Benki hii msiishie hapa kwa Vijana bali huu uwe ni mwanzo wenye uendelevu kwa kubuni bidhaa zaidi za mikopo kwa Wanawake na Walemavu ili tuunge mkono juhudi za Serikali katika kupambana na umasikini,” alisema Meya Rahibu

Meneja Mkuu wa Benki ya KCBL Bw. Godfrey Ngura amesema Benki hiyo itaendelea kuhakikisha kuwa inatoa huduma zenye malengo ya kugusa maisha ya watu kwa kuwawezesha kutoka kwenye hatua moja kwenda hatua bora zaidi kiuchumi. Akiongeza kuwa Benki ina dhamira ya kuona Wananchi wengi wanapata huduma za kifedha kupitia Benki zenye tija zitakazoendelea kubadili maisha ya wananchi wengi.

“KCBL inafanya kazi ili kufikia lengo la kuona kila mwananchi anapata fursa ya kutumia mifumo rasmi ya kifedha, hivyo huduma hii ya mikopo ya Bajaji ni njia ya kuongeza mtaji na kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema Meneja Mkuu Ngura

Meneja huyo akiongea katika uzinduzi ameeleza kuwa KCBL imekopesha Bajaji mpya 22 zenye thamani ya Shillingi Millioni 140 kwa vijana katika Manispaa ya Moshi kwa lengo la kuwawezesha kuendelea kujiajiri kupitia biashara hiyo ya usafiri. Akiongeza mpango huo unafanywa na Benki hiyo kwa awamu ya pili na kuahidi kuwa ni mpango endelevu katika kuendeleza na kupanua fursa za ajira kwa vijana.

Kwa upande wake Katibu wa Waendesha Bajaji na Bodaboda Bw. Rashid Omari ameshukuru Benki ya KCBL kwa kuwawezesha vijana na amewataka vijana hao kuhakikisha wanatumia na kuvitunza vyema Vyombo hivyo vya Usafiri ili viweze kudumu kwa muda mrefu na kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Aidha, Katibu huyo amewataka vijana waliokabidhiwa Bajaji hizo kufuata Sheria za barabarani, kuwa na leseni Pamoja na vibali vyote vinavyohitajika kwa ajili ya biashara ya usafiri ili waweze kutekeleza majukumu yao vyema, kupata kipato na kuchangia pato la Taifa.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: