Na Rhoda Simba, Dar es salaam.


WAANDISHI wa habari za mitandao wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuandika habari zenye ukweli na weledi ikiwa ni pamoja na kutumia takwimu za uhakika katika kuandaa habari huku wakiacha kuandika vichwa vya habari visivyo na uhalisia ili kuvutia wasomaji.


Wito huo umetolewa leo Novemba 1 jijini hapa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Nukta Afrika, Nuzulack Dausen katika mafunzo ya uhakiki wa habari yaliyoandaliwa  na taasisi ya vyombo vya habari Tanzania, (Tanzania Media Foundation TMF)


Aidha amesema kwa sasa waandishi wengi wa habari za mitandao wanaandika habari zisizo na vigezo huku wakiacha masuala mengi muhimu ikiwemo takwimu, mizani na ukweli.


“Changamoto kubwa inayosababisha hali hiyo ni baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari vya mitandaoni kujali idadi ya watu wanaotembealea mitandao yao bila kuangalia kama habari walizoweka zinasaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii,


Na kuongeza kusema kuwa “kwa sasa wasomaji wa mitandao wameanza kuzikwepa taarifa zenye vichwa vya habari vya kuvutia ambavyo haviendani na uhalisia wa habari”amesema Dausen


Awali akifungua mafunzo hayo     Kaimu Mkurugenzi  mtendaji wa TMF Dastani Kamanzi amesema waandishi wa habari wanatakiwa kuwa na msingi wa awali,jumla na wakubobea katika uandikaji wa habari.


“Msingi wa uandishi wa habari ni ukweli hivyo ni  muhimu waandishi wa habari kuzingatia misingi hiyo kila siku mnapoandaa habari zenu”amesema Kamanzi.


Hata hivyo mafunzo hayo ya uhakiki wa habari yamewajumuisha waandishi wa habari kutoka  mikoa ya Mara,Mwanza,Shinyanga,Tabora,Dodoma,Arusha na Mbeya lengo likiwa ni kuwajengea uelewa na kujifunza namna ya kuandika habari zenye ukweli na matokeo chanya katika jamii.

Share To:

Post A Comment: