Jane Edward, ArushaWaziri wa Fedha na Mipango, Dk.Mwigulu Nchemba, amewaonya wakuu wa mashirika ya umma na taasisi binafsi nchini kuacha tabia ya kuwaingiliwa Wakaguzi wa ndani katika utekelezaji wa majukumu yao.


Dk.Nchemba, alitoa ovyo hilo jijini Arusha, wakati akifungua mkutano wa nane wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania(IIA).


Alisema kwamba wakaguzi wa ndani wamekuwa msaada mkubwa katika maendeleo ya nchi na wamekuwa wakiwasisitiza kuangalia kasoro zote zinazojitokeza kabla ya wakaguzi wa nje.


“Wakaguzi wa ndani hasa wa serikali wamekuwa na mchango mkubwa wa maendeleo kwa kuwa wapo ndani ya ofisi za umma na wanaweza kuzuia upotevu wa fedha katika mashirika na taasisi zao,”alisema Nchemba.


Aidha alisema awali Rais Samia akiwa anapokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG),alitoa mwelekeo wa serikali yake, kuwa wakaguzi wote wa hesabu za serikali hawapaswi kuficha kitu chochote bali wanatakiwa kukagua kwa ujasiri kwa ajili ya kulinda fedha za wananchi.


“Kiongozi wa taasisi yoyote hapaswi kuwatisha wale ambao wanaotakiwa kusimamia ukaguzi wa fedha za walipakodi wa Tanzania, hivyo nasisitiza kuwa kila kiongozi anatakiwa kuzingatia kauli ya Rais Samia akimweleza CAG kwamba hatakiwi kupepesa macho wakati wa ukaguzi bali anapaswa kuwa wazi na jasiri.


“Kauli ya Mheshimiwa Rais ni maelekezo kwa kila yeyote anayeitumikia serikali hii hivyo sitarajii kwamba atatokea kiongozi au mtu atakayekwenda kinyume na agizo hili.alisema Mwigulu”


Aidha alisema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imepanga kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kupeleka kwenye miradi ya maendeleo na matarajio ya Watanzania ni kuona matokeo chanya ya hizo fedha hivyo mafunzo waliyopewa wakaguzi hao yatasaidia kwenda kuzisimamia vizuri na kuthibiti mianya ya wizi wa fedha hizo.


“Sisi kama Wizara ya Fedha na Mipango tutaendelea kushirikiana kwa ukaribu na taasisi hii waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo na watumishi wengi wa kada hii wafanikiwe kupata mafunzo haya na kubadilishana uzoef,”aliongeza.


Mkurugenzi Mkaguzi wa Benki ya Maendeleo Tanzania(TIB),Christine Mbonya, alisema kuwa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Fedha kwa Wakaguzi wa ndani watakwenda kuyafanyia kazi kwa kuwa amewapa nguvu ya kufanya kazi kwa bidii, kwa maarifa zaidi na kwa kutokuogopa.


“Waziri Mwigulu ametueleza kwamba kitu chochote tutakacho kiuona au kubaini tuseme na kuwa wazi bila ya kuwa na hofu yoyote kwa kuwa Rais alisema wakaguzi tuseme kwa kile tutachokiona na sisi tupo tayari kusema kweli kwa kile tutachokibaini kwa kuwa serikali ipo pamoja na sisi.


“Tunaihakikishia serikali yetu kwamba tutaweza kufanya vizuri na sisi kama wakaguzi wa ndani tutakagua na kutoa ripoti za haki na zenye kukidhi vigezo vya kimataifa .alisema Mboya.


Rais na Mwenyekiti wa IIA,Anna Victor, alisema kuwa wamepokea vizuri kauli ya Waziri Dk.Nchemba kwamba wakafanye kazi bila ya kuwa na hofu na pale panapotokea kasoro waseme ukweli na kuweka wazi.


“Tamko hili tumelipokea kama wazo chanya kwa kuwa linatutia moyo sisi tuendelee kusonga mbele zaidi kwa kuwa kwa muda mrefu tumekuwa tuna tatizo ambalo limekuwa likizuia katika utendaji kazi wetu kwa uhuru.


Alisema agizo la Waziri limewapa faraja kubwa kwa kuwa limeonyesha kwamba wanakwenda kupata msaada kutoka ngazi za juu za serikali ili waendelee kutekeleza wajibu wao kwa uhuru kwa lengo la kuleta maboresho.


Mwisho

Share To:

Post A Comment: