Baada ya Wizara kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa chumvi wa mikoa ya Mtwara na Lindi mwanzoni mwa mwezi Agosti 2021, leo Waziri wa Madini, Doto Biteko amekutana na wadau wa chumvi na kukubaliana kuziondoa changamoto hizo.


Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Abdulkarim Mruma uliopo katika Ofisi za Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzanaia (GST), Waziri Biteko amewataka wawekezaji wakubwa wa Kampuni ya Neelkanth Salt Limited kutoa elimu kwa wakulima wadogo ili waweze kuzalisha chumvi bora itakayokubalika kutumika katika kiwanda chao na hivyo kuwaondolea changamoto ya soko.


Akizungumzia vyanzo vya malalamiko ya wakulima wa chumvi, Waziri Biteko amesema anapata malalamiko kutoka kwa wakulima wenyewe lakini pia anapata malalamiko kutoka kwa wawakilishi wa wananchi ambao ni wabunge  na kumsihi mwekezaji Neelkanth Salt  Limited kutatua changamoto hizo. 


“Natamani nyie muwe chachu ya wakulima wengine ili wakue na kuzalisha kwa faida ili kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima," Amesisitiza Biteko.


Katika kutatua changamoto ya wakulima kusafirisha chumvi mpaka kiwandani na kuelezwa kuwa chumvi haina ubora na kuikataa ilihali wameingia gharama ya kusafirisha haijakaa vizuri.


Waziri Biteko amemshauri mwekezaji Neelkanth Salt  kupeleka vifaa na wataalamu wa maabara sehemu ya mashamba ili chumvi ipimwe na kutambulika endapo inakidhi vigezo kabla ya kuisafirisha  hivyo kuwapunguzia manung'uniko wakulima wadogo.


Awali akiwasilisha malalamiko ya wakulima wa chumvi kwa wajumbe wa kikao, Makamu Mwenyekiti wa  Chama cha  wa wakulima wa chumvi nchini (TASPA) Hamisi Chilinga, amesema kuna mashamba 400 ya chumvi kwa mikoa ya Mtwara na Lindi ambapo wakulima wamevuna lakini wamekosa soko kutokana na mnunuzi Kneelkanth Salt Limited kutoikubali chumvi inayozalishwa na wakulima hao badala yake huagiza chumvi kutoka nje ya nchi.

 

Akifafanua kuhusu tuhuma hizo Mkurugenzi  wa kampuni ya Neelkanth Salt Limited Ahmed Said amesema ni kweli kwamba hawanunui chumvi  kwa wakulima  kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kiwanda chake kutokuwa na uwezo wa kutenganisha kati ya chumvi na mchanga pamoja na kukidhi vigezo vya ubora wa chumvi inayozalishwa zinazokubalika na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).


Ameendelea kusema, kuanzia mwezi Aprili mpaka sasa wamenunua kiasi cha tani 2277 za chumvi na kubainisha chumvi ya wakulima iliyonunuliwa  ina mchanga ambapo kati ya tani 200 za chumvi alizonunua tani 20 sio nzuri.


Amesema miaka ya nyuma walikuwa wakinunua chumvi kutoka kwa wakulima lakini miaka 3 iliyopita kutokana na uhaba wa chumvi kwa wakulima iliwalazimu kuagiza chumvi kutoka India.


Ahmed ametoa wito kwa wakulima wa chumvi wenye nia ya kuzalisha   chumvi bora kufika na kupata elimu ya kilimo cha chumvi katika mashamba yao na kuahidi kuwaandalia usafiri, malazi na chakula kwa siku zote za mafunzo.


Akifafanua uwekezaji wa kilimo cha chumvi Mtendaji wa Kampuni ya NeelKanth Salt Limited Kumar Pujaro amesema uzalishaji wa chumvi unategemea hali ya mvua, kiwango cha uvukizi (evaporation rate) pamoja na hali ya upepo.


Pujaro amebainisha kuwa mahitaji ya juu ya chumvi kwa Tanzania hayazidi tani laki mbili kwa mwaka na kusema soko la chumvi ambayo haijaongezewa thamani linazidi kupungua siku hadi siku.


Aidha, uongozi wa Neekanth Salt Limited umekiri kuanza mara moja utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika kikao hicho ili kuiondolea changamoto Serikali ya kupokea kero za wakulima mara kwa mara.


Kikao hicho ni matokeo ya ahadi iliyotolewa wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya katika mikoa ya Lindi na Mtwara mwanzoni mwa mwezi Agosti iliyolenga kusikiliza changamoto za wawekezaji wa sekta ya madini na kuahidi kufanyia kazi malalamiko ya wakulima wa chumvi. 


Pamoja na Waziri wa Madini Kikao hicho kiliwashirikisha Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mulabwa na wataalamu wengine kutoka wizarani, Uwakilishi kutoka Tume ya Madini,  Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), wawakilishi wa Chama cha Wakulima wa Chumvi nchini (TASPA),  uongozi wa juu wa mnunuzi na mmiliki wa kiwanda cha chumvi cha Neelkanth Salt Limited,  Mkurugenzi wa kiwanda cha chumvi cha Nyanza Salt.

Share To:

Post A Comment: