Mkuu wa wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amefungua rasmi mafunzo ya vijana wa Jeshi la akiba (Mgambo) yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kaiho, kijiji cha Rwigembe, Kata ya Ngenge , wilaya ya Muleba ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kuimarisha Uzalendo, Ulinzi na Usalama wa Taifa letu. 


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Toba Nguvila aliwapongeza vijana hao kwa kuwa na moyo wa utayari kuweza kuhudhuria mafunzo hayo na kuwataka wawe wadadisi kwa mambo ambayo watafundishwa na wakufunzi wao pamoja na kuwa na jitihada binafsi ili waweze kufuzu mafunzo hayo.


"Nichukue fursa hii kuwaasa kwamba katika kipindi hiki chote cha mafunzo muwe na nidhamu nzuri, muwe watiifu, wasikivu na muwe wadadisi juu ya mambo ambayo mtafundishwa na wakufunzi wenu ili muweze kufuzu. Na ili muwe na mafanikio lazima muwe na jitihada binafsi hivyo ziangatieni sana kile mtakachofundishwa ili mfaulu mafunzo haya" alieleza Mhe. Toba Nguvila.


Aidha, amewapongeza wakufunzi na wanafunzi kwa ujumla kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kufyatua tofali zaidi ya elfu ishirini na tano (25000) ambazo zitatumika kujenga vyumba vinne vya madarasa.


Pamoja na hayo Mhe. Toba Nguvila amesisitiza uwepo wa upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi mashuleni kuwa ni makubaliano ya wilaya na kwamba kuanzia sasa watoto wapewe chakula kitakachowawezesha kushiriki katika masomo yao kikamilifu.


Aidha, Mshauri wa Jeshi la Akiba Luteni Issa Malesa ameeleza kuwa mafunzo haya ya Jeshi la Akiba ni sehemu ya utaratibu wa Jeshi na mahali ambapo mafunzo hufanyika huwa wanaacha alama chanya katika eneo hilo. Hivyo kwa awamu hii wamefanikiwa kufyatua tofali zaidi ya elfu ishirini na tano (25,000) ambazo zitatumika katika ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa. Pia amewaahidi vijana watakaofaulu mafunzo hayo kuwatumia katika masuala ya ulinzi na katika shughuli mbalimbali ikiwemo mradi wa bomba la mafuta ambao utapita kwenye eneo la kata ya Ngenge. 


Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngenge Mhe. Fidelis Kamugisha amewashukuru vijana wa mafunzo ya Jeshi la Akiba kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kufyatua tofali yatakayosaidia katika ujenzi wa vyumba vya madarasa huku akieleza kuwa Mbunge wa jimbo la Muleba Kaskazini, Mhe. Charles Mwijage amechangia mawe tripu 12 na mchanga tripu 6.


Mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwaandaa vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za ulinzi na usalama wa Taifa letu bila kujali itikadi.Ambapo katika mafunzo hayo vijana hao watajifunza juu ya usalama wa raia na mali zao, mbinu za kivita, mbinu za kupambana na majanga ya moto, kulinda nchi dhidi ya wahamiaji haramu na masuala ya kuzuia na kupambana na Rushwa.


Mafunzo yana jumla ya wanafunzi 65 ambapo vijana wa kike ni 7 na vijana wa kiume 58.


Imetolewa na: 


Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,

Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.

Share To:

Post A Comment: