Na. Angela Msimbira TAMISEMI


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshugulikia Afya Dkt. Grace Magembe amewaagiza waratibu wa huduma za maabara wa mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanazifungia maabara bubu zinazoendeshwa kinyume na utaratibu katika maeneo yao 


Akifunga Kikao kazi cha waratibu wa Huduma za Maabara  wa Mikoa na Halmashauri leo Jijini Dodoma Dkt Magembe  amesema  kuwa maabara bubu kwa sasa hazitakiwi kuwepo kwa kuwa kwa sasa Serikali imejipanga kuhakikisha inatoa huduma bora za afya kwa jamii


Amesema inashangaza kuona kuna viomgozi mbalimbali katika ngazi ya Kata, Halmashauri na Mkoa lakini bado kunakuwa na maabara bubu, timizeni majukumu yenu kwa kuhakikisha maabara hizo zinafungiwa kwa kuwa zinachafua taaluma ya maabara nchini.


 Amewataka kuhakikisha maabara zote nchini zinasajiliwa na kutambulika na Serikali na wafanye kazi wakiwa na wataalam wenye ujuzi,weledi  na kutoa vipimo ambavyo vinasaidia kuwapa matibabu wananchi.


“Zoezi hili la kuzikagua Maabara Bubu ziendane sambamba na maabara za Watu binafsi, pamoja na maabara za Serikali, kwa kuwa maabara zote zinatakiwa kufanyakazi kwa kuzingatia vigezo na masharti ya kitaaluma” amesisitiza Dkt Magembe


Kuhusu kero za Wananchi amewataka kuhakikisha wanashughulikia kero za wananchi kwa kuwasikiliza na kusimamia utoaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini 


Dkt. Magembe amewataka kuhakikisha wanasimamia utoaji wa huduma  bora kwa wananchi kwa kuangalia umahiri wa watumishi wa maabara ili kujua taaluma zao na uwezo wao katika kutoa huduma hiyo kwa jamii, kwa kuwa serikali inahitaji kutoa huduma bora kwa kutoa vipimo  sahihi.

Share To:

Post A Comment: