Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) kuanzia sasa yatafanyika katika mkoa mmoja ili kuhakikisha kuwa wakulima na wanaushirika wanapata fursa ya kutumia maadhimisho hayo kukutana na wadau mbalimbali kwa lengo la kupanua wigo wa kuongeza tija na masoko.

Akizungumza katika Ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yalianza leo Jumanne, Juni 29,2021 katika Viwanja vya Nanenane Mkoani Tabora hadi kufikia kilele chake Julai 3, 2021, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema kuanzia mwaka huu na miaka miwili itakayofuata yatafanyika mkoani Tabora

Naibu Waziri ameeleza kuwa kufanyika kwa Maadhimisho hayo katika Mkoa mmoja kutawezesha ushirika katika mkoa husika kuongeza fursa za Kilimo na biashara kwa kuwa Ushirika na biashara ni masuala yanategemeana.

Akielezea Kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho hayo isemayo “tujijenge upya kwa ubora na tija” amesisitiza kwamba Viongozi na watendaji wa kuwa Vyama vya Ushirika wanahitaji kuongeza uwajibikaji wenye uadilifu na unaozingatia maadili ya kazi. Wakati huohuo amepongeza hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa katika kudhibiti mianya ya ubadhilifu ambazo zimekuwa zikionesha kuanza kupungua kwa vitendo vya ubadhilifu.

“Kutokana na Juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali yetu wakati tukitathmini Siku 100 tangu kuingia madarakani Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan tunaona vitendo vya ubadhilifu katika baadhi ya maeneo yameanza kupungua ndio maana tunaona kuna mabadiliko kwenye Ushirika” alisema Mhe. Bashe

Naibu Waziri ameongeza kuwa Mchango wa Sekta ya Kilimo katika Uchumi lazima uonekane na Vyama vya Ushirika vikiwekeza katika tija vitasaidia sana kuinua maisha ya wakulima. Aliongeza kuwa Sekta ya inatoa ajira kwa wananchi wengi takribani asilimia 60 hadi 80 wameajiriwa kupitia Sekta ya Kilimo na kusisitiza kuwa Kilimo kikitumika vyema kitakuwa nyenzo ya kuondokana na umasikini nchini.

Aidha, Mhe. Bashe ameshauri Vyama vya Ushirika vyenye maeneo yenye wakulima wanaolima mazao aina nyingi kujishughulisha na mazao zaidi ya mmoja badala ya Chama kuwa na shughuli za kimsimu peke yake ili kuongeza tija ya uzalishaji na uchumi wa wakulima wao.

“Naomba Msianzishe utitiri wa Vyama kama eneo linazalisha mazao mengi basi Vyama vya Ushirika vilivyopo katika eneo hilo lihudumie wakulima waliopo hapo tusifikie kuanzisha Vyama kabla hatujatumia ipasavyo vile vilivyopo,” alisisitiza Naibu Waziri

Kwa upande wake Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege amesema lengo la Maadhimisho hayo ni fursa kwa Umma kujua masuala ya Ushirika na faida zake, changamoto wanazopitia wanaushirika na mikakati iliyopo ya kuimarisha ushirika.

Mrajis ameeleza kuwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuhamasisha Vyama vya Ushirika kuhusu umuhimu wa upatikanaji wa huduma za ugani na pembejeo kwa wanachama kwa wakati kupitia Vyama vya Ushirika.Akiongeza kuwa uhamasishaji huu umekuwa ukifanyika ili kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinaajiri maafisa Ugani katika Vyama vyao ili kusaidia wakulima.Hadi kufikia mwezi Februari 2021, Vyama vikuu vya ushirika vimeajiri maafisa ugani 75 ambao wameendelea kutoa huduma za ugani kwa wakulima katika mazao ya tumbaku, Korosho na Kahawa.

Dkt. Ndiege amebainisha kuwa Vyama vya Ushirika viliagiza kupitia mfumo wa ushirika mbolea tani 22,175 zenye thamani ya Shillingi 6,018386,364 mbegu na viwatilifu tani 252 vyenye thamani ya Shillingi 860,645,250, mbolea tani 17,237.44. Mrajis ameongeza kuwa uhamasishaji wa matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi ghalani pamoja na huduma za Ushirika Afya kwa wakulima.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: