Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto imetoa fedha za kujenga kiwanda cha dawa chenye uwezo wa
kuzalisha dawa kwa siku mbili ili kuondoa uhaba wa dawa uliopo na
kupunguza bajeti ya dawa zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi.
Hayo
yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee a Watoto Dkt. Godwin Mollel wakati akiongea na kituo kimoja cha
runinga hapa nchini.
Mhe.Samia Sulluh Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ameshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha
kuzalisha dawa nchini kitachosaidia kuboresha huduma za afya nchini kwa
kuongeza upatikanaji wa hali ya dawa na kupunguza matumizi ya fedha
ambazo zingetumika kununua dawa nje ya nchi.
“Rais Samia Suluhu
Hassan ametoa fedha, sasa kinajengwa kiwanda kule Njombe ambacho
kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge maana yake ni kwamba bidhaa za
Dawa zitashuka bei, dawa ambayo ilikuwa inanunuliwa mara moja
itanunuliwa mara mbili mpaka mara tatu.” Alisema Dkt. Mollel.
Aliendelea
kusema kuwa, hali ya huduma za afya inaendelea kuwa bora nchini hususan
katika upatikanaji wa dawa, kwani Serikali imeendelea kutenga fedha za
kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa ili kukabiliana na uhaba uliokuwepo
katika kipindi cha nyuma, huku akiweka wazi kuwa, Serikali imeshatoa
Bilioni 123 kiasi kilichotoka kabla ya Bajeti ya mwaka huu.
“Kwa
kipindi kifupi cha Rais, mama yetu Samia Suluh Hassan alivoingia kwenye
Mamlaka, tumepata kiasi cha shilingi Bilion 123 kwaajili ya dawa, hizo
ni fedha zilizotoka ndani ya muda mfupi kabla ya hii Bajeti mpya ambayo
tumeifanya, ambayo lengo lake ni kwenda kuimarisha suala la Dawa, Vifaa
tiba na Vitendanishi.” Amesema Dkt. Mollel.
Kwa upande mwingine
amekiri kuwa, Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa
wananchi kuhusiana na dawa, huku akiweka wazi kuwa tayari Waziri wa Afya
Dkt. Dorothy Gwajima ameshapokea mrejesho kutoka kwa timu ya ukaguzi
aliyoichagua kwenda katika hospitali za mikoa na utekelezaji wake
unaanza kufanyiwa kazi ili kudhibiti mianya yote ya upotevu wa dawa
nchini.
“Ni kweli kumekuwa na malalamiko mengi kuhusiana na suala
la dawa, mmesikia Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gajima ameunda timu
zimeenda kwenye hospitali zetu zote za mikoa na wameleta mrejesho, sasa
suala la upatikanaji wa dawa sio suala tu la fedha, ukiangalia Serikali
imekuwa ikitoa mabilioni ya fedha, mwaka uliopita ilitoa Bilioni 270,
ikatoa Bilioni 220 tena, kwahiyo tatizo la upatikanaji wa dawa sio la
fedha tu bali uwadilifu na uwazi kwa baadhi ya watoa huduma lakini pia
suala la uelewa kwa wananchi.” Alisema
Kwa upande mwingine Dkt.
Mollel amesema kuwa, Serikali inaendelea kumalizia mchakato wa Bima ya
afya kwa wote, utakaosaidia kila mwananchi kuweza kupata huduma bora
katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini jambo
litakalosaidia kurahisisha matibabu kwa wananchi.
“Tukienda kuwa
na Bima ya Afya kwa wote, maana yake kwenye eneo la afya tunaenda
kufanya kila Mtanzania aweze kupata huduma bora za Afya, lakini tunaenda
kuondoa tatizo ambalo limekuwa likilalamikiwa siku zote la upatikanaji
wa dawa liwe limetatulika.” Alisema.
Hata hivyo, ameweka wazi
kuwa, Bajeti yenye weledi mkubwa iliyopitishwa na Bunge ina msaada
mkubwa sana katika Sekta ya afya, huku akiweka wazi kuwa bajeti ya Sekta
zote kwa kiasi kikubwa zina akisi sekta ya afya, mfano sekta ya maji ni
muhimu katika utoaji huduma katika vituo, sekta ya mawasiliano na
miundombinu.
“Serikali inapowekeza kwenye sekta nyingine, maana
yake ni kwamba Sekta ya afya nayo inaguswa moja kwa moja, mfano Wizara
ya Afya inapojipanga kupunguza vifo vya mama na mtoto, wakati mwingine
inafika mahali tunagawa simu vijijini ili kuhakikisha uwepo wa
mawasiliano ili kumuokoa mama mjamzito.” Alisema
Post A Comment: