Na John Walter-Mbulu

Kutokana na wanafunzi waishio kata ya Sanu iliyopo wilayani Mbulu Mkoani Manyara kutembea umbali mrefu kwenda shuleni, wananchi wa kata hiyo wameamua kuchashingishana kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ili kuhakikisha watoto wao wanaondokana na adha wanayoipata.

Wananchi hao kutoka katika mitaa nane za kata hiyo wameitikia wito wa diwani wa Sanu Peter Sulle kuchanga fedha na vifaa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari.

Akizungumza wakati wa harambee maalum kwa ajili ya changizo hilo, Sulle ambaye pia ni mwenyekiti wa Halmshauri ya mji wa Mbulu na mwenyekiti wa ALAT mkoani hapo, amesema shule hiyo itakapokamilika  wanafikiria kuipa jina mojawapo kati ya Samia Sekondari au Ndalichako Sekondari kutokana na jitihada zao kwenye sekta ya elimu nchini.

Hata hivyo,amewaomba wadau wengine wa maendeleo  kutoka maeneo mbalimbali kuwaunga mkono kwa kuchangia ujenzi huo  ambao mara utakapokamilika utachangia   kuongeza morali ya kujisomea na kupanda taaluma  kwa wanafunzi.

Kwenye harambee hiyo pamoja na ahadi jumla ya Shilingi Milioni 11,040,400  zilipatikana.

Sulle amesema Kata  hiyo  haikuwahi kuwa na shule ya Sekondari kwa miaka yote na wakati anagombea udiwani sehemu ya ahadi yake ilikuwa ni kujenga Sekondari na kuwaahidi wananchi kutowabana kwa michango ile ya kisheria na badala yake kutumia Ubunifu ili kujenga shule bila kuwaumiza kwa michango mikubwa kupitia harambee na michango ya marafiki.

"Kwa hiyo baada ya kupata udiwani nilianza kazi hiyo  kama ambavyo inaonekana  na madarasa hayo sita yanayoonekana yamejengwa kwa muda wa siku 33 na natarajia mwaka 2022 wanafunzi kuanza kusoma katika shule hii" Sulle

Alisema kwenye kikao kuhusu maendeleo ndani ya kata  aliwashirikisha  mipango ya kuitisha harambee ya watu wachache na kufanikiwa kupata shilingi milioni 11 kutoka kwa marafiki huku  wengine wakileta mawe,mchanga na kokoto.

Amesema  fedha hizo  zilitumika kununulia nondo,saruji zilizowezesha kujenga madarasa sita hadi  hatua ya lenta, ofisi mbili za walimu na matundu manne ya choo.

Amesema Kazi hiyo imefanyika kwa kipindi cha muda mfupi kutokana na ushirikiano alioupata kutoka kwa wananchi ambapo kupitia wenyeviti wa mitaa walitoa matofali.

Pia aliendelea kusema alifanikisha hilo kwa kufanya mikutano ya uhamasishaji kwa kumuomba kila mmoja katika kata ya Sanu achangie shilingi elfu tano  (5000) huku wengine wakichanga shilingi elfu mbili (2000).

Hata hivyo amesema kitu ambacho wanakosea viongozi wengi ni kukosa ubunifu hali inayopelekea kuwa na michango mingi inayoumiza wananchi.

Alisema anategemea kuwa na harambee kubwa zaidi ya hiyo ambayo itasimamiwa na Mbunge wa mbulu mjini na kuwashirikisha viongozi wengine katika mkoa wa Manyara.

Amesema dhana ya kuwashikrikisha wananchi katika shughuli za maendeleo ni suala ambalo ni muhimu na kwamba  mara nyingi viongozi wanachokosea ni kusimama katika sheria  bila kuangalia utofauti hasa wa viwango vya mapato kwa wananchi.

"Kwa mfano katika harambee hii nimekaa vikao na mitaa nane inayounda kata ya Sanu na kuzungumza nao kwamba nyinyi mnafikiri tufanyeje ambapo walishauri kuwepo kwa harambee ambayo kila mmoja atashiriki,nina amini Sanu wata enjoy wakati wangu huu" alisema Sulle 

 Amewashauri viongozi wengine kubadilika kwa kufuata dhana ya ushirikishwaji katika shughuli za maendeleo kuliko kutumia mifumo wa kisheria hatua inayopelekea kuvutana na wananchi na hata kuwapeleka kwenye vyombo vya dola.

Aidha amewakumbusha viongozi kuwa wawazi kwa wananchi kwa kusoma mapato na matumizi katika shughuli zote zinazohusu fedha bila kujali zimetokana na nini.

"Shuguli za maendeleo hazitaki kutumia nguvu na ubabe,zinahitaji watu kukaa na kukubaliana" Sulle

Pamoja na hayo diwani huyo amesema anatarajia kukutana na kuzungumza na viongozi wa dini kuwaomba mchango ili kukamilisha ujenzi wa shule hiyo.

Madiwani wa kata 17 za Halmashauri ya Mji wa Mbulu wamemuunga mkono diwani mwenzao kwa juhudi zake za kujenga shule ambapo diwani wa viti maalum tarafa ya Nambis  Dorcas Mlewa, alisema hatua hiyo itawaondolea adha wanafunzi ya kutembea umbali mrefu waliyokuwa wakiipata  hasa wasichana ambao hukumbana na vikwazo vingi bara barani.

Akizungumza na waandishi wa katika eneo la ujenzi, Afisa elimu kata ya Sanu John Leonard amesema kutokana na ukosefu wa shule wanafunzi hulazimika kutembea umbali kilomita sita hadi saba kwenda shule zilizo jirani na kata hiyo hivyo ujenzi ukikamilika utakuwa umesaidia wanafunzi kusoma karibu.

Amempongeza diwani huyo kwa hatua aliyoichukua na kusema huo ni  mfano mzuri wa kuigwa na wengine ili kuendeleza na kukuza elimu nchini.

Wananchi wa kata hiyo wamempongeza diwani kwa hatua hiyo huku wakisema kuwa hawakukosea kumchagua.

Tangu kuanzishwa kwa kata hiyo hadi leo hakuna shule ya Sekondari hivyo ujenzi huo wa shule ukikamilika itakua ndo shule ya kwanza ya Sekondari katika kata hiyo yenye mitaa nane.

Share To:

Post A Comment: