Katibu Tawala Msaidizi Uchumi Bw. Ellias Luvanda (kulia) akikabidhi tuzo ya kutambua utendaji mzuri katika uagizaji wa Mbolea kwa pamoja iliyotolewa na Mamlaka ya Mbolea TFRA , akimkabidhi Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Iringa (IFCU) Bw. Victor Mwipopo (kushoto) wakati wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho mkoani Iringa

Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akieleza jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama hicho mkoani Iringa

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 20 wa Chama Kikuu cha Ushirika IFCU Wakifuatilia taarifa wakati mkutano huo ukiendelea


Viongozi wa Vyama vya Ushirika wamepewa wito kusimamia matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani ili kuhakikisha wakulima wanapata masoko ya mazao yao na bei zenye tija kwa kuweka vipaumbele vya mipango ya ujenzi wa maghala kuanzia ngazi ya vijiji.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu tawala Msaidizi Uchumi Elias Luvanda wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 20 wa mwaka wa wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Iringa IFCU (1993) Ltd, uliofanyika Ijumaa Mei 07, 2021 Mkoani Iringa.

Katibu Tawala Msaidizi Luvanda amesema Serikali inahamasisha na kuendeleza wakulima kwa kuhakikisha Mfumo wa Stakabadhi ya Ghalani unaimarika. Hivyo, amewataka Viongozi katika mkutano huo kuweka mipango yenye malengo ya kuongeza maghala ya kuhifadhi mazao ya wakulima ili kukabiliana na changamoto ya uchache wa maghala na kuzingatia matumizi bora ya maghala.

Aidha, amewataka viongozi wa Ushirika kuwa wasimamizi wazuri wa rasilimali za Vyama vya Ushirika, kuwajibika kwa wanachama wao kwa kufuata misingi na taratibu za Ushirika zitakazosaidia kuondokana na matumizi mabaya ya mali iza vyama pamoja na ubadhilifu.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea kwa niaba ya wanaushirika amesema Vyama vya Ushirika vitaendelea kutoa ushirikiano na kuvitaka Vyama vya Ushirika kuanzia ngazi ya Vyama vya msingi kutimiza wajibu wao Kiushirika kama vile kuandaa makisio, kufanya mikutano mikuu ya mwaka pamoja na kuhakikisha wanachama wanalipa hisa za chama. Hivyo, kuwezesha Chama kikuu kufanya kazi vizuri na hatimaye mfumo wote wa Ushirika kutimiza wajibu wake.

“Wanachama wa Ushirika ndio wamiliki wa Vyama vya Ushirika hivyo viongozi wa Ushirika mnawajibika kwa wanachama wenu kuhakikisha mnatoa taarifa za utendaji, taarifa za fedha na maendeleo ya Vyama kupitia mikutano pamoja na matakwa mengine ya Sheria ya Vyama vya Ushirka Na.6 ya mwaka 2013,” alisema Mrajis

Aidha amewataka wajumbe wa Mkutano kusoma taarifa zinazotolewa na kuhoji pale inapobidi kuhusu masuala ya uendeshaji wa Chama chao kwani Mkutano Mkuu ndio ngazi ya juu ya maamuzi ya Chama

Hakikisheni mnafuatilia taarifa zitakazoendelea katika Mkutano huu pale mnapoona hamridhiki mna haki ya kuhoji, kupata majibu pamoja na kupitisha makisio na baada ya hapo Mrajis Msaidizi wa Mkoa na Maafisa Ushirika wanaidhinisha kwa mujibu wa Sheria.

Mrajis amewataka Viongozi wa Vyama vya Ushirika kuwa wabunifu kwa kubuni miradi mbalimbali yenye tija na maendeleo kwa Vyama vyao. Akiongeza kuwa ni muhimu Wanachama wa Ushirika waweze kupata thamani ya kujivunia vyama vyao kupitia huduma za Vyama zitakazowatofautisha wanachama na wasio wanachama wa Ushirika.

“Tuhakikishe kuwa ndani ya Vyama vya Ushirika wakulima wanapata huduma bora kama vile upatikanaji wa pembejeo kwa bei nafuu na kwa wakati, elimu ya ushirika, bima ya afya, masoko na bei nzuri za mazao,” alisisitiza Mrajis

Mrajis ameeleza kuwa dhana ya Ushirika ndio njia ya kuinua Uchumi wa watu wengi kwa pamoja hivyo ni muhimu kuzingatia utendaji wenye kuzingatia maadili na taratibu za Ushirika ili kulinda uendelevu wa Vyama na kujenga uchumi imara wa wananchi wanyonge.

Dkt. Ndiege amevitaka Vyama vyote vya Ushirika ambavyo vimepata hati chafu kwa mujibu wa Shirika la Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) kufanya jitihada mahususi za kuondokana na dosari zilizosababisha hati hizo chafu. Alibainisha baadhi ya sababu za hati hizo ni kukosa elimu ya uandishi wa vitabu, utunzaji mbovu wa kumbukumbu na mengine.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: