Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kuwa imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuitangaza Hifadhi ya Taifa  ya Katavi ili iweze kupata watalii wengi na kuongeza mapato.


Akizungumza leo Bungeni Jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mary Masanja wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu Mhe. Martha Festo lililokuwa likihoji kuwa Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Katavi, amesema serikali kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Katavi waliandaa mpango mkakati wa kukuza Utalii katika  mkoa huo  mwaka 2019 na  umesaidia kwa kiwango kikubwa kuitangaza hifadhi hiyo.


Amesema Hifadhi hiyo imekuwa ikitangaza Vivutio vya Utalii  kupitia Vyombo mbalimbali vya habari vya  ndani ya nchi na nje ya nchi ikiwemo mitandao ya kijamii kwa kuwa ni miongoni mwa  Hifadhi zenye viboko,simba na twiga weupe.


Kwa upande wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Damasi Ndumbaro amesema serikali ina mpango mkakati wa kushirikiana na Halmashauri zote, Serikali za mitaa na Wilaya kuutangaza utalii ikiwemo kuwatumia wabunge kutangaza vivutio vya  utalii vilivyopo katika maeneo yao.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: