Na Elizabeth Joseph,Arusha.


Jamii yaombwa kuacha kuchinja Punda na kutumia ngozi ama nyama yake kwakuwa sheria ya Ustawi wa wanyama ya mwaka 2008 namba 19 na kanuni zake inamtambua Punda kuwa ni mnyama kazi hivyo ni kosa kisheria kuendeleza vitendo hivyo.


Hayo yamesemwa na Afisa Elimu Ustawi wa Wanyama Diana Msemo kutoka Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na Ustawi wa Wanyama(ARUSHA SOCIETY FOR THE PROTECTION OF ANIMALS-(ASPA) la mkoani Arusha wakati wa semina ya siku moja iliyoandaliwa na Shirika Hilo kwa Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha juu ya umuhimu wa kumlinda Punda pamoja na kutambua haki zake.


Alisema kuwa Punda ni mnyama anayeshika nafasi ya 2 katika kuchangia pato la taifa kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kutokana na kazi anazofanya hivyo jamii inatakiwa kumthamini kwa kumtimizia haki zote kama wanyama wengine.


"Punda amekuwa msaada mkubwa kwa maisha ya binadamu hasa za kifugaji kutumika katika kazi mbalimbali za kiuchumi hasa ubebaji wa mizigo na anashika namba mbili katika kuchangia pato la taifa ukiacha ng'ombe hii ni kwa mujibu wa Tafiti iliyofanywa na TARIRI "alisema Afisa huyo.


Aliongeza kuwa kwasasa wafugaji wengi wamekuwa na changamoto ya wizi wa Punda pamoja na utoroshwaji wa Wanyama hao kwa kuwapeleka Mkoa wa Shinyanga pamoja nchi jirani ya Kenya ambapo wao wana viwanda vya kuchakata nyama na ngozi ya Wanyama hao.


"Kenya kulikuwa na viwanda vinne vya kuchakata nyama na ngozi y Punda ambavyo mwanzoni mwa mwaka Jana vilifungwa ila vilifunguliwa wiki moja iliyopita mwaka huu kwakuwa wale wawekezaji walishinda kesi iliyokuwa imefunguliwa...........


"Upande wa Longido,Monduli,Tarakea, Same bado wimbi la usafirishaji wa Punda linarudi tena,hii ni changamoto kubwa hivyo serikali iliangalie hili kwa jicho la pekee ili kuzuia vitendo hivi"alisisitiza Bi Msemo.


Naye Mkurugenzi wa ASPA Livingstone Masija aliiomba serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanya sensa maalum ili kujua idadi ya Punda nchini ikiwa ni pamoja na kuweka sheria ndogondogo za kulinda Wanyama hao ili kuzuia wasipotee kutokana na vitendo vya uuzaji wa nyama na ngozi yao.


Aidha aliitaka jamii nchini kumthamini Punda kutokana na  msaada wanaoutoa katika maisha ya kila siku ikiwemo kuchota maji,kulima na kubeba mazao mbalimbali.


"Kama ilivyo kwa Wanyama wengine Punda wanahitaji  kupatiwa chakula,maji na matibabu kwaajili ya Magonjwa mbalimbali ambayo mengine hutokana na vidonda vilivyotokana na uzito wa mizigo wanayobeba...........


"Unakuta punda anabeba mzigo ambao haulingani na uzito wake lakini hatibiwi vidonda vinavyomtokea wala kupewa chanjo ila anaongezewa majukumu ya kubeba mzigo siku hadi siku hali inayochangia vifo kwao na hata ongezeko la Magonjwa mengine kupitia vidonda vile"aliongeza Masija.


Mwisho.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: