Naibu Waziri wa maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akizungumza na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Amanimakolo kata ya Amanimakolo wilayani Mbinga alipokuwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika majimbo ya Mbinga mjini na Mbinga vijijini.

WAKAZI wa kijiji Kipapa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, wameishukuru wizara ya maji kupitia wakala wa  usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) kufikisha huduma ya maji safi na salama.


Wakizungumza jana mbele ya naibu waziri wa maji Maryprisca Mahundi wamesema, awali walipata shida kubwa ya kukosa maji safi,hali iliyosababisha kuhatarisha afya zao kwa kutumia maji kutoka kwenye vyanzo ambavyo sio salama.

Basilius Komba alisema, watahakikisha wanatunza miradi na miundombinu yote ya maji na kuwachukulia hatua  watu  wanaofanya shughuli za kibinadamu  ikiwemo kilimo na kuchungia mifugo kwenye vyanzo ya maji.

Pensia Kowelo alisema,awali walilazimika kwenda mbali kufuata maji kwa matumizi yao ya kila siku jambo lililorudisha nyuma maendeleo yao kwa kuwa walipoteza muda mwingi kwenda kutafuta maji badala ya kushiriki katika kazi za maendeleo.

Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini Benaya Kapinga, ameipongeza wizara ya maji kukamilisha ujenzi wa miradi ya maji ambayo imemaliza kero ya wananchi  wa jimbo hilo kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji.

Hata hivyo,ameiomba Serikali kuhakikisha inatoa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji  katika jimbo hilo ili ziweze kukamilisha miradi iliyoanza kujengwa na wananchi wafaidi matunda ya serikali yao.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa maji Maryprisca Mahundi amewataka wananchi kuacha kufanya  shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji ili kulinda vyanzo hivyo na miundombinu ya maji inayojengwa kwa gharama kubwa.

Alisema, serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya  ujenzi wa miradi ya maji na kuwapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa kuendelea kushirikiana na serikali kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema, wizara ya maji  imedhamiria kutekeleza na kukamilisha miradi  yote ya maji ili kumaliza kero  kwa wananchi ambao wanalazimika kutumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwa matumizi yao ya kila siku.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri,serikali tangu ilipoanzisha wakala wa maji vijijini Ruwasa imepunguza kwa asilimia kubwa kero ya upatikanaji wa huduma ya maji hapa nchini  na kuwataka wananchi  kuwa  na imani na serikali yao.

Ametoa wiki moja kwa meneja wa wakala wa maji vijijini Ruwasa wilaya ya Mbinga na meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma kuhakikisha wana maliza tatizo la kutojaa  maji haraka kwenye moja ya tenki linalotumika kusambaza maji kwa wananchi wa kijiji hicho.
Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: