Na. Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
MAREKANI imeahidi kushirikiana na Tanzania kukuza mitaji na kuvutia uwekezaji kutoka nchini humo ili kuchochea zaidi uchumi na huduma za kijamii hapa nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Marekani hapa nchini Dkt. Don Wright, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ofisini kwake Jijini Dodoma

“Uhusiano wa Tanzania na Marekani ni imara na umedumu kwa zaidi ya miaka 60 sasa, ni wajibu wangu kuendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano huu kwa kuwahamasisha wawekezaji wengi zaidi kutoka Marekani kuja kuwekeza teknolojia na mitaji yao hapa nchini” alifafanua Dkt. Wright.

Mhe. Balozi Don Wright ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu, ameainisha maeneo mengine ya kipaumbele kwamba ni kuwekeza na kuimarisha sekta ya afya pamoja na kuanzisha program ya kusaidia vijana wa Kitanzania kwa kuwajengea uwezo, ujuzi  na maarifa ili kukuza maarifa yao pamoja na ajira.

“Kwa miongo kadhaa sasa Marekani imekuwa ikishirikiana na Tanzania kupambana na maradhi kama vile ukimwi, kifua kikuu, malaria, kutekeleza program za uzazi wa mpango, masuala haya tutayaimarisha zaidi” aliongeza Dkt. Wright

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa  Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amemhakikishia Mheshimiwa Balozi Wright, kwamba Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na kumshukuru Balozi huyo kwa kuahidi kuwahamasisha wawekezaji wengi kutoka Marekani kuja kuwekeza hapa nchini.

Alibainisha kuwa kunapokuwa na uwekezaji mkubwa nchini kutachochea mitaji, ajira, pamoja na kuwa chanzo cha kukuza sekta nyingine zinazozalisha malighafi zinazotumika viwandani na vile vile kitakuwa chanzo cha kodi zitakazosaidia kutekeleza miradi ya maendeleo na kusisimua uchumi wa nchi.

Ameeleza pia kuwa mambo mengine waliyojadili na mgeni wake ni namna ya kuboresha mkataba wa ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani hususan masuala ya misamaha ya kodi kwenye misaada inayoletwa na Marekani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini, baada ya Serikali kubaini kuwepo kwa udanganyifu wa baadhi ya mashirika kutumia vibaya misamaha hiyo, serikali iliweka zuio.

Alimwahidi balozi huyo kwamba Serikali itapitia upya mkataba huo kwa kuwashirikisha wataalam wa pande zote mbili ili walete mapendekezo ya namna ya kufanya kwa lengo la kutokwamisha upatikanaji wa misaada hiyo pamoja na namna ya kuziba mianya ya matumizi mabaya ya misaada hiyo iliyokuwa inafanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu.

 “Kuna maeneo ambayo sisi kama Serikali tumepanga kuyaangalia ili tusikose misaada kutoka kwa wenzetu kwa sababu ya kuwadai kodi kwenye misaada wanayoyotupa na kwa kufanya hivyo tunakosa kodi pamoja na misaada iliyokuwa ielekezwe kwenye miradi ya maendeleo, tunapoikatalia” alisema Dkt. Nchemba.

Kuhusu suala la kuwasaidia vijana, Dkt. Nchemba aliishukuru Marekani kwa kudhamiria kuleta program ya kusaidia kundi hilo kwa kutengeneza taasisi zinazoweza kuwaandaa vijana kujiajiri, jambo linalowakabili wahitimu wengi.

Mwisho 
Share To:

msumbanews

Post A Comment: