Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewataka wamiliki wa ardhi nchini kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho vya taifa kwani wizara hiyo ina mpango wa kuanza kuwatambua wamiliki wote wa ardhi kwa kuwasajili upya kupitia vitambulisho hivyo ili kudhibiti watu wanaotumia majina hewa kujilimbikizia viwanja vilivyopimwa.

Akizungumza wakati wa zoezi la ugawaji wa leseni za makazi katika halmashauri ya jiji la Mwanza, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Dk.Angelina Mabula ameongeza kuwa zoezi la urekebishaji wa taarifa za umiliki wa ardhi kupitia kitambulisho cha taifa litakuwa ni la muda maalumu.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Mwanza Elia Kamihanda amesema kupitia programu maalum ya wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, jumla ya vipande vya ardhi 5,957 vimeshatambuliwa huku Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba akielezea namna leseni za makazi zitakavyoleta tija kwa wananchi.

Baadhi ya wanufaika wa mpango wa kupanga, kupima na kumilikisha vipande vya ardhi bila kujali maeneo waliyopo wamesema kupitia mpango huo ardhi zao zimeongezwa thamani na kueleza mipango yao ya baadaye mara baada ya kupata leseni za umiliki wa maeneo hayo.

Share To:

Post A Comment: