Mwandishi wetu,


Aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Simanjiro mkoani Manyara,James Ole Milya ameibuka na kuzungumzia ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa fedha za serikali(CAG) ya mwaka 2019/20 na kusisitiza kuwa akiwa bungeni aliwahi kulalamikia shirika hilo kupata hasara Mara kwa Mara lakini hakueleweka.


Katika ripoti ya CAG iliyowasilishwa Jana mbele ya Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan shirika la ndege la Air Tanzania (ATCL) limeonekana kuendeshwa kwa hasara ya kiasi cha sh,60 bilioni.


Akihojiwa na waandishi wa habari Ole Milya alisema kwamba kelele kuhusu shirika hilo kuendeshwa kwa hasara zimepigwa tangu bunge lililopita lakini wakati akilalamika alionekana kichaa.


Alisema kwamba uamuzi wa serikali kununua ndege haukuwa mbaya lakini tatizo lilikuwa ni namna shirika  linavyojiendesha.


"Hizi kelele kuhusu shirika la ndege kupata hasara tulishazipiga muda mrefu nikiwa bungeni rejeeni hotuba zangu zilizopita lakini Mimi nilisema kwamba serikali haikufanya uamuzi mbaya kununua ndege tatizo ni namna linavyojiendesha" alisema Ole Milya 


Hatahivyo,Ole Milya alisisitiza kwamba baadhi ya wanasiasa serikalini hawakumshauri vizuri hayati Rais John Magufuli kuhusu namna ya kuendesha shirika hilo na kupelekea hasara za Mara kwa Mara.


"Ukiangalia katika ripoti ya CAG ya mwaka 2018/19 shirika lilipata hasara kubwa tu na ripoti ilipoletwa bungeni Mimi nilizungumza lakini baadhi ya washauri wa hayati  Rais Magufuli walikuwa hawamshauri vizuri" alisisitiza Ole Milya


Hatahivyo,alizungumzia hatua ambazo Rais Samia amezichukua kwa sasa kupambana na ufisadi na kudai kwamba endapo akisisimamia vizuri huenda akabaini madudu mengi katika kipindi cha muda mfupi.


Ole Milya alipongeza hatua zinazochukuliwa na Rais Samia kwamba zimeonyesha nia ya uzalendo na kupambana na rushwa huku akiwataka watanzania wamuunge mkono.


"Rais Mama Samia anaonekana ni mtu aliyenyooka na mwaminifu nakwambia akiendelea kusimama imara atabaini wizi mkubwa tu sisi kama watanzania tumuombee na tumuunge mkono" alisema Ole Milya


Mwisho.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: