Na Tito Mselem Dodoma,


Imeelezwa kuwa, kufuatia Marekebisho yaliyofanywa katika Sheria ya Madini ambayo ni Matunda ya jitihada za aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli yameipaisha Tanzania na kuifanya iheshimike kimataifa.


Hayo yamebainishwa leo Machi 22, 2021 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi wakati akitoa Wasifu wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.


Marekebisho na Sheria ya Madini yaliyokuwa yakisisitizwa na aliyekuwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli yameifanya Tanzania kunufaika na rasilimali zilizopo nchini humo.


Aidha, Prof. Kabudi amesema kukamilika kwa ujenzi wa Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani, umesaidia kuthibiti utoroshwaji wa Madini ya Tanzanite ambapo kwa sasa ulinzi wake umeimarika na hivyo kuongezeka kwa mapato yatokanayo na madini hayo.


Pia, Prof. Kabudi amesema, Rais Magufuli kwa ujasiri na uthubutu wake amesaidia kuhakikisha Serikali inapata asilimia 16 za hisa kutoka kwa wawekezaji wanaochimba nchini na lengo likiwa kufikia asilimia 50 jambo ambalo ni la kizalendo kwa nchi yake.


Sambamba na hilo, Prof. Kabudi amesema, kutokana na maelekezo ya Hayati Dkt. Magufuli, yalianzishwa masoko kila Mkoa ambayo yameongeza ukusanyaji wa Mapato ya Serikali yatokanayo na Rasilimali Madini.


Naye, Uhuru Kenyata, Rais wa Kenya amesema, Hayati Magufuli amesaidia kwa kiwango cha juu kuhakikisha Tanzania haitegemei msaada kutoka nje ya nchi na badala yake alihakikisha rasilimali zilizopo nchini zinatumika katika kuiletea maendeleo Tanzania.


Pia, Rais Kenyata, ameihakikishia Tanzania kuendelea kushirikiana na Kenya na kuleta maendeleo ya Tanzania, East Afrika na Afrika kwa ujumla.


“Rais Mwenzangu Samia Suluhu Hassan, Dkt. Magufuli amekuonesha Barabara, amekufungulia barabara, hivyo wito wangu kwako ni kuchapa kazi kama ilivyo kauli mbiu ya hapa kazi tu na Watanzania wote niwaombe mumuunge mkono Rais wenu Samia Suluhu ili ayafanye kikamilifu yale aliyoyaacha Dkt. Magufuli,” aliongeza Rais Kenyata.


Katika shughuli hiyo ya kumuaga Dkt. John Pombe Magufuli, aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imehudhuriwa na Maraisi 12 na Ujumbe mbalimbali kutoka kwa Marais walioshindwa kufika katika shughuli hiyo.


Baadhi ya Marais waliohudhuria ni pamoja na Rais wa Kongo, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Rais wa Kenya, Rais wa Jamhuri ya Zambia, Rais wa Jamhuri ya Botswana, Rais wa Msumbiji, Rais wa Zambia, Rais wa Zimbabwe, Rais wa Malawi, Rais wa Sri Lanka pamoja na Rais wa Zanzibar.


Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewapongeza watanzania wote kwa kuonesha hali ya utulivu katika kumuaga aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.


Pia, Rais Samia amesema ataendeleza mazuri yote aliyoyaacha Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kuwataka Watanzania wamuamini kwani anao uzoefu na weledi wa kutosha.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: