Askofu Kiongozi wa Kanisa la ABC, Flaston Ndabila


Na Dotto Mwaibale


ASKOFU Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Center (ABC) la Tabata  Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo wamempongeza  Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Sita wa Tanzania.

Mbali na pongezi hizo Askofu Ndabila ametumia nafasi hiyo kumpa pole Rais Samia Suluhu Hassani kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt.John Magufuli kilichotokea jana Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam kwa ugonjwa wa moyo.

Wengine waliyopewa pole ni mjane wa marehemu Janeth Magufuli, viongozi mbalimbali na watanzania wote kwa ujumla.

Ndabila akimzungumzia Hayati Rais John Magufuli alisema watanzania watamkumbuka kwa mambo yote ya maendeleo aliyofanya.

"Kila ninapofikiria mambo ambayo Mungu alimpa neema Rais wetu Magufuli kuyatenda nakumbuka vile Bwana yetu Kristo alivyo kuwa akifanya kazi zake hapa duniani." alisema Ndabila.

Ndabila akimtolea mfano Yesu  wakati akifanya kazi zake za kitume yalitokea mabishano mengi kati yake na waandishi , wanasheria, mafarisayo na masadukayo. 

" Kwa kuwa mtindo wake Yesu  wa kufanya kazi ulitofautiana kabisa na mazoea yao wengine walimtuhumu hafuati taratibu na desturi zao ambazo zilikuwa ni kinyume na mazoea yao ambapo aliokota fimbo na kuwapa mkong'oto na kupindua meza zao walipokuwa wakifanya biashara haramu hekaluni wakati alisaidia watu siku ya sabato na kuponya huku akiwaambia wale aliowaponya wabebe magodoro waende zao kumbe walikuwa  wakikwazika." alisema.

Ndabila alisema Yesu aliwajibu watu hao waliokuwa wakishindana naye kuwa kazi za mtu humshuhudia, kazi za mtu humsadikisha kwa watu. kazi za mtu humuaminisha mtu.

Alisema Rais wetu Magufuli ambaye Mungu amemtwaa alituaminisha ya kwamba kazi anazozifanya anazifanya kwa kumtanguliza Mungu na kuwa mafanikio yake yanatokana na  kumuweka  Mungu mbele.

" Magufuli aliwaaminisha watanzania kumwamini Mungu kwa kila kazi wazifanyazo na kuwa wakati wote alikuwa upande wake" alisema Ndabila.

 Alisema kitendo hicho cha kuwaaminisha kiliwapa wepesi wa kufundisha neno la Mungu na kuwa kazi hizo zilipokuwa zikifanyika alimrudishia Mungu utukufu.

Alisema maaskofu watamkumbuka  Magufuli kwa kuwapa  ari ya  kazi  baada ya kuona kiongozi wao ambaye ni mkuu wa nchi akimtanguliza Mungu kwa vitendo na ameondoka huku kazi zake zikiwa zinahubiri na kushuhudia.

Ndabila   alisema Rais Magufuli atakumbukwa kwa kazi kubwa alizozifanya katika kipindi chake kifupi cha uongozi wake.

" Kazi  aliyofanya   ni ya kutukuka ukiangalia hapa Dar es Salaam na mikoani ni mahali  gani utaenda usione mabadiliko kuanzia barabara, madaraja ya juu kuanzia Tazara na Ubungo" alisema.

Ndabila alisema mbali ya kazi hizo amejenga stendi kuu za mabasi za kisasa katika ya mikoa ya Simiyu,Morogoro, Korogwe Tanga, Kibaha na Dodoma pamoja na vituo vya afya, Hospitali na shule ukiachilia mbali miradi mikubwa kama  Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Reli, ununuzi wa vivuko kwa ajili ya usafiri wa majini, ndege na mingine. 

Share To:

Post A Comment: