Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Maalim Seif Sharif Hamad (77) ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo amefariki dunia leo Jumatano Februari 17, 2021 saa 5:26 asubuhi.
Akihutubia Taifa kwa njia ya televisheni, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amesema Maalim Seif alifariki dunia akiwa katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa tangu Februari 9, 2021.
Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi ametangaza siku saba za maombolezo kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad.
Mwanasiasa mkongwe Maalim Seif amefariki dunia akiwa ametumikia wadhifa wa makamu wa kwanza wa rais wa SMZ kwa chini ya siku 100 - akiwa sehemu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020.
Kifo chake kinahitimisha safari ya kisiasa ya mwanasiasa mashuhuri kuliko wote wa Zanzibar na kiongozi ambaye alizibeba siasa za upinzani katika visiwa hivyo katika muda wa miaka 30 iliyopita.
Post A Comment: