Na Angela Msimbira SUMBAWANGA 


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe David Silinde amewaagiza Viongozi wa Mikoa yote nchini kuhakikisha zoezi la ujenzi wa madarasa linakuwa endelevu na kuwekewa mikakati maalum ili kupunguza uhaba wa madarasa nchini.


Ametoa agizo hilo leo wakati akikagua  miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Mkoani  Rukwa ambapo  Mhe. Silinde amesema zoezi la ujenzi wa madarasa si la kushitukiza, hivyo ni vyema viongozi wote ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kuweka mikakati madhibuti ya kuhakikisha madarasa yanajengwa kwa wakati.


“Haiwezekani kila mwaka tunajua idadi ya wanafunzi wanaomaliza  elimu ya msingi lakini bado tunakuwa na uhaba wa madarasa nchini, hali hii inapoteza  haki ya watoto waliofaulu vizuri mitihani yao  ya kumaliza elimu ya msingi  kukosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza” amesisitiza Mhe. Silinde 


Mhe. Silinde  anafafanua  kuwa Serikali itahakikisha inakagua na kujiridhisha utoshelevu wa madarasa kwa watoto wote waliofaulu Mitihani ya kumaliza shule ya msingi na kuwa watahakikisha kuwa wanapangiwa shule.


Amesema Serikali hahitaji maneno mengi kinachohitajika ni kuwa madarasa yamekamilika, kwa kuwa,   watoto kujiunga na Kidato cha kwanza si jambo la dharura, hili ni jambo linalofahamika katika kipindi chote, hivyo udharura huihitajiki katika miaka mingine inayokuja “amesisitiza Mhe. Silinde


Mhe Silinde amesema kuwa zoezi la ujenzi wa madarasa linatakiwa kuwa endelevu na kuhakikisha kuwa hakuna uhaba wa madarasa kulingana na wanafunzi wote wanaoongezeka kila mwaka.


“Inafahamika kuwa kunaongezeko kubwa na wanafunzi kila mwaka, wanafunzi wanaofuatia kwa mwaka mwingine, pia ongezeko la idadi ya watu kila mwaka katika taifa letu, hivyo kila Mkoa uhakikishe unajipanga na kuweka mikakati madhubuti ya kutatua tatizo la madarasa” amesema mhe. Silinde 


Mhe. Silinde ametoa Rai maeneo yatakayoonekana na upungufu mkubwa wa madarasa, vifaa ikiwemo madawati Serikali haitasita kuwachukulia hatua viongozi wa eneo hilo kwa kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.


Ameendelea kufafanua kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inafuatilia na kuhakikisha hakuna muda wa kupumzika katika kipindi chote mpaka watoto wote waliofaulu na kuchagulliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanasoma  madarasani


Wakati huohuo  Mkuu wa Wilaya ya Sumabawanga  Mhe. Halfani Haule   amesema  mpaka sasa Halmashauri hiyo imejipanga kukamilisha maboma ya madarasa yaliyopo  lengo likiwa kuhakikisha  watoto waliofaulu elimu ya msingi wote wanachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na wanakaa darasani


Naye Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Wilaya ya  Sumbawanga  Mwl. Nyangi Msema kweli amesema kuwa Halmashauri hiyo imetenga kiasi cha shilingi  milioni 57 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya shule ili kuhakikisha wanafunzi zaidi ya 4400 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wanaingia darasani ifikapo januari, 2021.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: