Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo akinguzumza na Wathibiti Ubora wa Shule na watumishi wapya (hawapo pichani) wakati wa akifunga mafuzo ya kuwaingiza kazini watumishi hao yaliyofanyika mkoni Morogoro mwishoni mwa wiki.
Baadhi ya watumishi wapya na Wathibiti Ubora Shule wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo wakati akifunga mafunzo ya kuwaingiza kazini watumishi hao yaliyofanyika mkoni Morogoro mwishoni mwa wiki.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na Wathibiti Ubora wa Shule na watumishi wapya mara baada ya kufunga mafuzo ya kuwaingiza kazini watumishi hao yaliyofanyika mkoni Morogoro.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewaagiza Wathibiti Ubora wa shule kuhakikikisha Shule zote za Msingi na Sekondari zinakuwa na Kamati na Bodi zinazofanya kazi kwa mujibu wa sheria za elimu.
Agizo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki Mkoani Morogoro na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo wakati akifunga mafunzo ya kuwaingiza kazini watumishi wapya pamoja na Wathibiti Ubora wa Shule ambao wamehamia makao Makuu ya Wizara ambapo amesema kuwepo kwa bodi katika shule za sekondari na kamati kwa upande wa shule za msingi ni utekelezaji wa sheria ya elimu Sura Na.353 (RE 2002)
Dkt. Akwilapo amesema zipo shule ambazo zimekuwa zikiendeshwa bila ya kuwa na Kamati au Bodi jambo ambalo linapelekea kuwa na changamoto katika uendeshaji, akitolea mfano shule ya Right Way ambayo imejidhihirisha kutokuwa na Bodi ya shule na kuleta usumbufu wakati wanafunzi wakijiandaa kufungua shule Juni 29, 2020.
“Hivi karibuni mmiliki wa Shule ya Right Way ya Mbezi Beach Dar es Salaam, ameonesha dharau kwa wazazi, Kamati ya shule na hata mamlaka za nchi. Hatuwezi kuwadekeza wamiliki wa shule kama hawa. Anasema hawezi kuitisha kikao cha wazazi na hana Kamati ya shule, hii ni kinyume kabisa na taratibu na kanuni. Ni jukumu lenu Wathibiti Ubora wa Shule kwenda kuwaelekeza wamiliki wa shule ili wajitambue na waelewe namna walivyo na jukumu kubwa katika kuelimisha jamii,” amesema Dkt. Akwilapo.
Aidha, Dkt. Akwilapo amewataka Wathibiti Ubora Wakuu wa Kanda na Wilaya kuchukua jukumu la kuhakikisha walimu wote wa shule binafsi wanafanyiwa uhakiki kama ilivyofanyika kwa watumishi wa sekta ya umma pamoja na kuhakikisha ratiba za masomo zinazingatiwa.
“Tumepata malalamiko mengi sana kuhusiana na ratiba za masomo, kuna shule zinaanza masomo alfajiri saa 12 sasa unajiuliza huyu mtoto anaamka saa ngapi ili afike muda huo na wengine wanabakizwa shuleni mpaka saa 12 jioni hii sio sawa wathibiti mkaangalie na hilo,” alisema Dkt. Akwilapo
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Akwilapo amewataka Wathibiti Ubora wa shule waliopata mafunzo kuhakikisha wanafuata kanuni na taratibu katika utendaji pamoja na  kutumia busara na hekima katika utoaji wa maamuzi.
“Busara na hekima ndio nyenzo kubwa kwenye utumishi wa umma. Ni kweli tuna sheria na kanuni lakini mwisho wa siku Kiongozi unatakiwa utoe hukumu kwa hekima na busara huku ukiangalia mazingira yaliyopo,” aliongeza Dkt. Akwilapo.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya kuingia kazini ambaye pia ni Mthibiti ubora wa shule Kanda ya Dar es Salaam, Alodia Ndumbaro amesema mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kufanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa kwani uthibiti ubora ni jicho la jamii ambalo linapaswa kuona changamoto zilizopo kwenye maeneo ya kazi wanayosimamia na kusaidia kutafuta ufumbuzi hivyo kuboresha utendaji kazi.
Share To:

Post A Comment: