Kaimu mkuu wa Wilaya ya Busega, David Pallangyo, amewataka wananchi kutoa ushirikiano na kuacha fikra potofu juu ya zoezi hilo. Amesisitiza kuwa dawa zinazotumika katika zoezi hilo la kuua mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria hazina madhara yoyote kwa afya ya binadamu hivyo wananchi watoe ushirikiano ili kukamilisha kusudio la zoezi hilo.
Awali Mganga Mkuu wa Wilaya ya Busega Dkt. Godfrey Mbangali, akimkaribisha mgeni rasmi amesisitiza kuwa zoezi hilo la kupulizia dawa kwenye mazalia ya mbu lililofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la T-Marc Tanzania wanaoshughulika na mradi wa badili tabia tokomeza Malaria kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto litafanyika kwenye kata zote 15 kwa siku nne, na litahusisha sehemu zenye maji yaliyotuama ambazo ndizo sehemu kuu za mazalia ya mbu wa malaria.
Ugonjwa wa Malaria ni moja ya magonjwa yaliyo na maambukizi makubwa wilayani Busega. Kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2018 hali ya maambukizi ya Malaria kwa jamii ya Busega ilikuwa ni 8.3% ambayo ilikuwa ya pili kimkoa kuwa na maambukizi ya juu, huku katika kipindi cha miaka mitatu maambukizi ya Malaria kwa wilaya ikiwa 45,719. Hivyo kuzinduliwa kwa zoezi hilo kutasaidia kupunguza maambukizi ya malaria wilayani Busega.
Post A Comment: