Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwatumia wataalam wa sekta ya ardhi waliopo kwenye ofisi za ardhi za mikoa katika kupanga na kupima ardhi katika halmashauri zao.

Lukuvi alisema hayo jana wakati akizindua ofisi za ardhi za mkoa wa Iringa ikiwa ni mfululizo wa uzinduzi wa ofisi za ardhi kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Waziri Lukuvi ambaye tayari alizindua ofisi za ardhi kwenye mikoa ya Tanga, Arusha, Manyara na Singida alisema, halmashauri nchini hazitakiwi kuwa na visingizo vya upungufu wa wataalamu wa sekta ya ardhi kuwa wataalam hao sasa wanapatikana ofisi za ardhi za mikoa.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, watumishi wa sekta ya ardhi waliopo ofisi za ardhi za mikoa wanaweza kutumiwa na halmashauri mbalimbali za wilaya hasa pale panapokuwa na uhitaji wa wataalam hao katika masuala ya kupanga na kupima maeneo mbalimbali yakiwemo mashamba na vijiji.

‘’Hawa watumishi ni wa kwenu, watumieni msipowapanga na kuwatumia hawana kazi tushirikiane’’ alisema Lukuvi

Alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo kuanza mchakato wa kuwapanga upya watumishi wa sekta ya ardhi kwenye halmashauri za wilaya nchini baada ya kukamilika zoezi la awali la kupeleka watumishi kwenye ofisi za ardhi za mikoa.

Akizungumzia suala la utoaji hati za ardhi nchini, Lukuvi alisema baada ya kuanzishwa ofisi za ardhi za mikoa anategemea upatikanaji hati sasa hautakuwa na usumbufu tena kwa wananchi kwa kuwa huduma hiyo inapatikana karibu.

Alibainisha kuwa, hati pamoja na nyaraka mbalimbali zilizokuwa kwenye ofisi ya ardhi ya kanda mkoani mbeya tayari zimerejeshwa Iringa ambapo alitolea mfano wa hati 238 ambazo wamiliki wake walishindwa kuzifuata mbeya zimerejeshwa mkoani Iringa.

Aidha, Waziri Lukuvi alisema pamoja na mkoa wa Iringa kuwa na viwanja 37,220 vilivyoidhinishwa kupatiwa hati ni wamiliki 14,473 pekee waliojitokeza kuchukua hati na kufanya zaidi ya wamiliki 20,000 kutochukua hati na kuikosesha serikali mapato yatokanayo na kodi ya ardhi.

Kufuatia hali hiyo, Lukuvi amewaagiza maafisa ardhi kuhakikisha wale wote waliokamilisha taratibu za upimaji na kuwekewa mawe katika viwanja vyao kupelekewa hati za malipo na kupatiwa hati za viwanja vyao ndani ya wiki moja kuanzia Julai mosi mwaka huu.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Happi alisema, sekta ya ardhi ilikuwa na shida sana katika mkoa wake na kubainisha kuwa uanzishwaji ofisi ya ardhi katika mkoa huo ni faraja kwake na wana Iringa kwa ujumla kwa kuwa ile kazi ya kuitisha jalada la ardhi kutoka mbeya  haitakuwepo tena.

Aliwataka wana irnga kuitumia fursa ya kuwepo ofisi ya ardhi katika mkoa wao katika kutoa huduma za sekta hiyo na wakati huo kuzitaka hlamashauri kutokuwa na kisingizo cha kuchelewesha hati za ardhi.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema, uanzishwaji ofisi za ardhi katika mkoa wa Iringa ni mkombozi kwa wananchi wa mkoa huo kwa kuwa hivi sasa hawatapata usumbufu wa kufuata huduma katika umbali mrefu na huduma zote kama vile Upimaji, Upangaji, Uthamini na utoaji hati utapoatikana kwenye mkoa wa Iringa.
Share To:

Post A Comment: