Jesse Chonde -Kigoma
Taasisi za ubunifu zilizo chini ya wizara ya Viwanda na biashara zimetakiwa kubuni mashine zitakazosaidia uvunaji na uchakataji wa mafuta ya mawese ili kuongeza thamani ya zao hilo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe alito agizo hilo mkoani Kigoma wakati wa ziara ya kuangalia uzalishaji wa zao la michikichi ambalo ni moja ya mazao ya kimkakati ya Taifa.

Katika ziara hiyo Prof.Shemdoe alipata fursa ya kutembelea vitalu vya michikichi katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo kilichopo eneo la Kihinga na Gereza la Kwitanga zilizopewa jukumu la upandaji na usambazaji wa mbegu zinazotoa mafuta kwa wingi aina ya TENERA.  

“Nimeona namna miche inayozalishwa kwa wingi, hivyo naziagiza taasisi za SIDO, CARMATEC, na TIRDO kubuni teknologia za   kuongeza uzalishaji wa mafuta yenye kukidhi viwango vya ubora”

Aliongeza kuwa hadi sasa zao la michikichi ndiyo linaloongoza kwa uzalishaji wa mafuta ya kula kwa wingi duniani likifuatiwa na mazao mengine. Hivyo alizitaka taasisi hizo kuwekeza katika teknolojia za kisasa kwa ajili kuvuna,kukusanya na kuchakata mazao ya michikichi. Hii inafuatia juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali katika kusimamia upandaji wa miche bora ya michikichi yenye uwezo wa kutoa mafuta mengi ikilinganishwa na miche iliyokuwepo awali.


Kwa upande wake Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Bi. Upendo Mangali alisema Halmashauri hiyo ina jumla ya wakulima 27,945 na jumla ya hekta 9177.8 zimepandwa miti ya michikichi ambapo asilimia sabini (70%) ni michikichi ya asili aina ya DURA na asilimia thelathini (30%) ni michikichi ya kisasa aina ya TENERA ambayo ina  uwezo wa kutoa kati ya kilo 4000 hadi 4500 za mafuta kwa hekta moja kwa mwaka.

Alisema wakulima wa michikichi wamekuwa wakitumia mashine ambazo hazina ufanisi hivyo aliomba upatikanaji wa mashine bora kufanyika kwa haraka.  

Alifafanua kuwa kugundulika kwa mbegu hizo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa fedha za taifa zilizokuwa zikitumika kuagiza mafuta ghafi kutoka nje ya nchi kwa ajili ya viwanda vya mafuta ya kula vilivyomo nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa michikichi -Kihinga Dkt. Filson Kagimbo alisema mpaka Juni 2020 kituo kimezalisha mbegu 1,805, 868 ambazo zinaweza kupanda eneo la ekari 36,117, Katika hizi asilimia 30% imechangiwa na sekta binafsi kwa makubaliano.

“Tunapoendelea na kuzalisha mbegu kwa wingi na kuzisambaza kwa wakulima, tuna uhakika baada ya muda uzalishaji wa mafuta ya maweze utakuwa mkubwa”, alisema Dkt. Kagimbo

Alitoa wito kwa wadau kuwekeza katika ubunifu wa mashine za kisasa kwa kuwa Mashine zilizopo kwa  sasa hazina ufanisi mkubwa kwa kuwa zina zinakamua mafuta kwa asilimia thelathini (30%) hadi asilimia sabini (70%), wakati duniani kwa sasa mashine zilizopo zina uwezo wa kukamua asilimia 90% na kuendelea ya mafuta kutoka katika mbegu.
Share To:

Post A Comment: