Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amekagua maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Chuo cha Ualimu Mpwapwa ambao umegharimu zaidi ya  Shilingi bilioni 2.8.

Akizungumza na wakufunzi, walimu na wanafunzi wa chuo hicho, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo, Profesa Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya Taasisi za Elimu ili kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu kwa watanzania.

Kiongozi huyo ametaja miundombinu inayojengwa kuwa ni jengo moja la ghorofa kwa ajili ya Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bweni la ghorofa moja la walimu tarajali wa kike, bwalo la chakula na nyumba mbili za watumishi ambazo nyumba moja ina uwezo wa kuchukua familia tatu.

“Serikali imeamua kwa dhati kuboresha miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ndio maana inawekeza katika eneo hili. Sasa ni jukumu lenu kusimamia na kuhakikisha miundombinu inatunzwa ili iweze kutumika kwa muda mrefu,” amesema Waziri Ndalichako.

Kaimu Katibu Tawala, Said Mwaliego akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo Jabili Shekimweri, ameishukuru Wizara kwa kupeleka kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa chuo hicho. Ameiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimamia mradi huo kwa karibu ili ukamilike kwa wakati.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Gerald Richard ameishukuru Wizara kwa kukipatia fedha za ukarabati chuo hicho kwani miundombinu yake ilikuwa imechakaa kutokana na kuwa cha muda mrefu, amesema ujenzi wa miundombinu unaoendelea utaongeza nafasi za udahili wa wanachuo wengi zaidi.
Share To:

Post A Comment: