Na John
Walter-Babati
Iwapo wewe
ni miongoni mwa watu ambao hulipa kodi ya zuio kwa ajili ya kupanga nyumba au
jengo la biashara, Serikali imesema mwenye nyumba anatakiwa kukurejeshea kiasi
cha fedha ulizolipa na si vinginevyo.
Hayo yamebainishwa
Bungeni jijini Dodoma baada ya Mbunge wa jimbo la Babati mjini, Paulina Gekul,
alipoihoji serikali kuwa ni lini
itabadili utaratibu wa kumtoza mpangaji
wa nyumba ya biashara kodi ya zuio ya asilimia 10 badala ya mpangishaji?
Akijibu swali la mbunge huyo, Waziri wa fedha na Mipango Dr. Philip Mpango
alisema “Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, mpangaji ambaye sio
mfanyabiashara na hajasajiliwa na TRA kama mlipakodi hapaswi kukusanya kodi
hii”.
Kwa mujibu
sheria za kodi nchini Tanzania mpangaji wa nyumba ya biashara husajiliwa na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwa wakala wa ukusanyaji wa Kodi ya Zuio
(Withholding Tax) hivyo kuwa sehemu ya mlipaji wa kodi ya pango.
Sheria ya
Kodi ya Mapato inamtaka mmiliki wa nyumba ya biashara mwenye
mapato yanayozidi Sh500,000 kulipa kodi ya zuio kutokana na mapato yanayotokana
na upangishaji wa pango (rental tax) kwa kiwango cha asilimia 10 ya mapato ya
kodi ya pango husika.
Hata hivyo baadhi ya wapangaji ambao hulipa kodi hiyo huwa
hawarudishiwi fedha hizo ambazo walitakiwa kukatwa wapangishaji ikiwemo hata
kufidiana kwenye kodi.
Dk. Mpango ameliambia Bunge kuwa kodi hiyo ya zuio siyo ya
mpangaji, na kwa kuwa Sheria ya Kodi ya Mapato inamtambua mpangaji kama wakala,
kiasi cha kodi ya pango ambacho kimelipwa na mpangaji huhesabiwa kama sehemu ya
fedha ambazo anapaswa kurejeshewa na mwenye nyumba.
Dk. Mpango amesema kuwa utaratibu wa ukusanyaji Kodi ya Zuio
kupitia wakala ambaye ni mpangaji umewekwa ili kurahisisha ukusanyaji wa kodi
hiyo, hususan pale mpangishaji anapokuwa hajasajiliwa na TRA kama mlipa kodi.
Post A Comment: