Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Idara ya  Uhamiaji mkoa wa Arusha imeshiriki katika kuhamasisha watanzania kutembelea hifadhi zilizoko nchini kwa kufanya ziara ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Tarangire ambapo wamejionea vivutio mbalimbali ikiwemo makundi makubwa ya tembo,twiga,pundamilia na vivutio vingine.

Afisa wa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Naibu Kamishna Abdallah Towo amesema kuwa wameamua kutembelea hifadhi ikiwa ni moja kati ya njia za kuhamasisha Taasisi nyingine za serikali kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi wakiwa na wafanyakazi wao lengo ikiwa ni kuhimiza ufanisi kazini na kujenga mahusiano bora kazini.

Mrakibu wa Uhamiaji  Issa Mlweta amesema kuwa licha ya kutembelea hifadhi hiyo uhamiaji ni wadau wakubwa wa utalii kwani wanawakaribisha watalii wanapoingia na kutoka katika mipaka ikiwa ni pamoja na kuhamasisha utalii na kutangaza vivutio muhimu tulivyonavyo.

Mhifadhi Mwandamizi  Ujirani Mwema  hifadhi ya Tarangire ,Harieli Msaki amesema kuwa hifadhi hiyo inatembelewa na watalii laki moja kila mwaka kutoka nchi za nje huku utalii wa ndani ukiwa chini hivyo ameipongeza uhamiaji na kuzitaka taasisi nyingine ziige mfano wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa tafiti na Maendeleo kutoka  Mega Media Group ,Hikloch Ogola ambao ni waandaaji wa ziara hiyo   amesema kuwa wameanzisha program maalumu ya kuhamasisha taasisi za umma na binafsi kutembelea vivutio vya utalii ili kuinua mapato ya utalii wa ndani na vile vile kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii..

Utalii ni moja kati ya sekta ambazo zinaongoza kwa kuliingizia taifa fedha za geni na kuchangia kiasi cha asilimia 17% katika pato la taifa hivyo juhudi endelevu zinahitajika katika kuhamasisha utalii wa ndani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: