Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini kuhakikisha wanawezesha maafisa elimu nchini kwa kutenga bajeti  kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao kikamilifu.


Ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Elimu Mikoa, Maafisa elimu maalum na maafisa elimu ya watu wazima kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha mipango, Jijini Dodoma.

Amesema kuwa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri hawatoi  kipaombele  katika masuala yanayohusu elimu maalum na elimu ya watu wazima katika Halmashauri zao jambo ambalo linafanya maafisa wa idara hizo  kuwa wanyonge na kukata tamaa ya kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

“Maafisa elimu wanaosimamia elimu maalum na elimu ya watu wazima  wako choka mbaya katika Halmashauri nyingi nchini, hata ukihesabu na kutaka viongozi wa Halmashauri wengi hawasimami kwa sababu ya kutojiamini na kujiona wametengwa na jamii hii inaleta sura mbaya na kusababisha watu walioko kwenye kundi hili kusahaulika  na kutotimiziwa mahitaji yao kwa wakati” Amesema Jafo.


Mhe. Jafo anafafanua kuwa maafisa elimu maalum  na elimu ya watu wazima hushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kutotengewa fedha na kuonekana si vipaombele vya Halmashauri, jambo ambalo linasababisha watoto wengi wenye mahitaji maalum na watu wazima kushindwa kupata elimu bora sawa na watu wengine.

“ Afisa elimu maalum akiwa na kazi maalum lazima aombe msaada wa gari kutoka Idara nyingine,hivyo nawaagiza wakurugenzi kuhakikisha katika bajeti zenu za ndani kutenga fedha kwa ajili ya maafisa elimu maalum na elimu ya watu wazima ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo” Amesisitiza Mhe. Jafo

Mhe. Jafo amewataka kuhakikisha wanaainisha vipaombele vya elimu maalum na watu wazima na kuviingiza katika bajeti ya Halmashauri husika ili kuziwezesha Idara hizo kupanga mipango yao na kuitekeleza kwa wakati.

Wakati huohuo, amemuagiza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha kila Halmashauri  inaainisha kwenye bajeti zao  vipaombele vya  Elimu Maalum na Elimu ya watu wazima  katika mchakato mzima wa bajeti  na kuwekewa fungu  katika Halmashauri zote nchini.

Amemtaka kuhakikisha anafanya uhakiki kwa kila mkoa pindi inapoleta bajeti yake kama wameweka vipaombele vya elimu maalum na elimu ya watu wazima, kama ilivyofanywa kwa asilimia kumi ya kuwawezesha vijana, wanawake na walemavu ili kuyafikia makundi hayo.

Mhe. Jafo amesema bila kufikia mahali na kuona ni kipaombele cha Halmashauri kuhakikisha kundi la watu maalum na elimu ya watu wazima linahudumiwa katika jamii, kundi hili litakuwa likitegemea wafadhili pekee jambo ambalo si malengo ya Serikali.

Vilevile amewaagiza maafisa elimu Maalum na watu wazima kuhakikisha wanatembelea maeneo yao ya kazi ili kutatua matatizo  ya kundi hili katika maeneo wanayofanyia kazi.


Naye, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema kuwa malengo ya mkutano huu ni  kuwapa uelewa Maafisa elimu kuhusu mpango mkakati wa elimu jumuishi kuwa ni ajenda muhimu katika maeneo yao ya kazi, kuwajengea uwezo wa namna ya kukuza na kusimamia maadili ya uongozi wa utumishi wa umma na dhana nzima ya ugatuaji wa madaraka na  kuendesha na kusimamia programme mbalimbali za maendeleo ya elimu nchini.

 Aidha, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia elimu Tixon Nzunda amewaomba wadau wa elimu nchini kuisaidia serikali kutekeleza majukumu yake katika kutatua changamoto mbalimbali za elimu nchini kwa kufuata vipaombele vinavyotolewa na kinyume chake watapingana na juhudi za Serikali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: