Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Steven Kebwe, ameiagiza Ofisi ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) mkoa, kuongeza vituo vya kutoa huduma hiyo katika wilaya zote ili kuwasaidia wananchi hasa waishio vijijini kupata huduma hiyo kiurahisi na kukamilisha katika muda mwafaka.

Dk. Kebwe alisema hayo wakati alipotembelea ofisi hizo kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi kuhusu kuchelewa kupata namba na vitambulisho jambo linaloleta athari za usajili wa laini za simu kwa jamii.

Alisema, licha ya kazi hiyo kuendelea, lakini bado miezi minne pekee kusitishwa kwa usajili wa laini za simu kwa alama za vidole mwezi Desemba mwaka huu, huku watu wengi wakiwa bado hawajapata.

Aliitaka jamii kuwa na mwamko wa kuitumia nafasi iliyopo ya kwenda kupata huduma hiyo kwa wakati kwa kuwa kuchelewa kunaweza kuleta usumbufu baadaye.

Rajabu Ally, mkazi wa  Manispaa ya Morogoro alisema, upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa  bado ni changamoto kutokana na vigezo au vielelezo na masharti vilivyowekwa ikiwamo mtu kutakiwa kuwa na cheti cha kuzaliwa au cheti cha shule hali inayowalazimu kufuatilia kwa kipindi kirefu bila ya mafanikio.

John Msekwa, mkazi wa Tungi alisema, serikali za mitaa zinatakiwa kuchukua nafasi yake kwa kuwatambua wakazi wa maeneo husika ili iwe rahisi kwao kupata vitambulisho bila kutegemea masharti yaliyopo.

"Nina miaka ya kuzaliwa zaidi ya 70 hapa, cheti nakipata wapi kwa sasa na nina mwezi wa sita natafuta kitambulisho, kitambulisho changu cha kupigia kura  kimeharibika sana, kila ninapokwenda wanagoma kunisajilia laini, sasa serikali ya mtaa ikisimama kwa hilo wengi tutapata vitambulisho," alisema.

Ofisa Usajili wa vitambulisho NIDA mkoani hapa, James Malimo alisema, kuchelewa kwa upatikanaji wa vitambuliso hivyo kwa baadhi ya wananchi kunatokana na wengi kushindwa kutimiza masharti yaliyowekwa na kwamba yapo maombi mbalimbali yamekwama kutokana na changamoto za wananchi kushindwa kuwasilisha vielelezo zaidi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: