Waziri wa Maliasili
na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla amewashukuru Madaktari, wauguzi na
wafanyakazi wa hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ya jijini
Arusha kwa huduma na matibabu waliyoyatoa kwake na kwa wasaidizi wake alipopata
ajali mbaya ya gari Agosti 4, 2018 katika eneo la Magugu mkoani Manyara.
Dk.
Kigwangalla ametoa shukrani hizo wakati akizungumza na Madaktari, Wauguzi na
wafanyakazi wa hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre, jijini Arusha.
Akiwa
ameambatana na mkewe Dk. Bayoum Awadh, amewashukuru na kuwapongeza madaktari na
wauguzi wa hospitali hiyo kwa matibabu waliyompatia kwa kipindi chote
alichokuwa hospitalini hapo na kuwaomba waendelee kuwahudumia wananchi wenye
shida.
Amesema
kazi ya udaktari, uuguzi na fani zote zilizo katika sekta ya afya ni za wito na
kila anayezifanya inampasa azifanye kwa wito kutoka ndani ya moyo wake.
“Kazi
ya udaktari, uuguzi na fani zote zilizo katika sekta ya afya kwa kiasi kikubwa ni
kazi ambazo mtu anazifanya kutoka ndani ya moyo wake kuwahudumia wengine ambao
wako katika madhira mbalimbali ya kiafya” Amesema Dkt. Kigwangalla.
Amesisitiza kuwa hakuna namna ambayo Daktari
au Muuguzi anayetoa huduma ya kumtibu mtu, kumwondolea maumivu, au kumpa faraja
mgonjwa anaweza kulipwa na malipo hayo yakalingana na kazi aliyoifanya.
Amesema
kazi ya Udaktari na Uuguzi inafanywa na watu wachache ambao kwa kiasi kikubwa
wanakua wameitika wito ama wametumwa na Mungu na kwamba mtu yeyote hawezi
kusema kuna kipato au kitu utakachoweza kumlipwa kikamtosheleza au kukidhi
umuhimu na ugumu wa kazi anayoifanya.
“Kwa
dhati ya moyo wangu ninatoa shukrani zangu za dhati lakini pia kwa niaba ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ambaye kwa muda
wote toka tulipopata ajali alikua akifuatilia afya zetu, ninaomba nifikishe kwenu
shukrani za Serikali anayoiongoza ya kwamba tunatambua mchango wenu mkubwa”
Amesisitiza Dkt. Kigwangalla
Ameeleza
kuwa yeye na wasaidizi wake waliopata ajali Agosti 4, 2018 walipita katika
hospitali hiyo wakiwa na hali ngumu kiafya lakini kutokana na juhudi na upendo
uliooneshwa na madaktari wa hospitali hiyo wakishirikiana na madaktari wa
hospitali ya mkoa wa Arusha na KCMC waliweza kushughulika afya zao na kuokoa
maisha yao.
“Tunawashukuru sana kwa yote mliyotenda,
tunawaombea dua madaktari, wauguzi na watumishi wa kada zote zilizo katika
sekta hii ya tiba hatuna cha kuwalipa zaidi ya kusema Mungu awabariki katika
maisha yenu, awape mafanikio makubwa na ujuzi zaidi ili muendelee kuwasaidia
wengine” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Kwa
upande wake Mkuu wa Idara ya magonjwa ya dharura cha Arusha Lutheran Medical
Centre (ALMC), Dk. Peter Mabula akizungumza kwa niaba ya uongozi wa hospitali
hiyo amesema kuwa kitendo cha Dkt. Kigwangalla kupanga muda wa kwenda
kuwashukuru kimewapa nguvu na moyo wa kuendelea kufanya kazi vizuri zaidi.
Dk.
Mabula amemwomba Mhe. Kigwangalla atenge muda mwingine wa kuitembelea hospitali
hiyo pia afikishe salam zao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwamba wataendelea kufanya kazi kwa
bidii na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Post A Comment: