RAIS Dkt. John Magufuli amesema Serikali itaendelea kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano.

Rais Magufuli amesema hayo leo tarehe 26 Aprili, 2019 ambayo ni siku ya maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano, wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Jiji la Mbeya katika uwanja wa Luanda, Nzovwe Jijini Mbeya akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi Mkoani hapa.

“Napenda kuwapongeza Waasisi wa Muungano wetu wakiongozwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kwa uamuzi wao wa busara.

Nataka kuwahakikishia kuwa tumejipanga kuulinda Muungano wetu na yeyote atakayethubutu kuuvunja atavunjika yeye” amesema  Rais Magufuli.

Katika mkutano huo Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa juhudi kubwa za uzalishaji mali hasa kilimo na amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Mbeya wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Albert Chalamila kwa kusimamia vizuri shughuli za maendeleo ikiwemo ukusanyaji wa mapato ambapo katika masoko ya Jiji la Mbeya mapato hayo yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 2.5 hadi shilingi Bilioni 5.

Rais amekubali ombi lililotolewa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Tulia Ackson ambapo ameagiza uwanja wa ndege uliopo Jiji Mbeya ubadilishwe matumizi na kuwa eneo la wafanyabiashara wadogo (Machinga), na ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuliboresha eneo hilo kwa kuweka huduma muhimu.

Aidha, Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kufuatilia ujenzi wa uwanja wa ndege wa Songwe ambao ujenzi wake unaonekana kuwa na dosari ili ukamilike haraka kwa viwango vya kimataifa na kuwezesha ndege za aina zote kutua na kuruka.

Kuhusu miundombinu ya Jiji la Mbeya, Rais Magufuli amesema Serikali imeanza mchakato wa kujenga barabara za mzunguko zenye urefu wa kilometa 40 ambazo zitasaidia kuondoa msongamano wa magari katikati ya Jiji na pia kusaidia kukabiliana na ajali zinazosababishwa na magari makubwa ya mizigo yaendayo nchi jirani kukatiza Jijini humo.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli ameagiza kuongezwa kwa muda uliowekwa kwa Watanzania kusajili laini zao za simu hadi kufikia Desemba mwaka huu na ameitaka Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuharakisha mchakato wa utoaji wa vitambulisho hivyo kwa Watanzania sambamba na usajili wa laini za simu kwa kuwa usajili wa laini hizo unafanywa kwa kutumia vitambulisho vya Taifa.

Rais ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kufuatilia kiwanda cha nyama cha Mbeya ambacho kilianzishwa enzi za Baba wa Taifa Hayati Mwl. Nyerere na baadaye kikatelekezwa.

Mapema kabla ya hotuba ya Rais Magufuli, Mawaziri walioongozana nae pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila wameeleza juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani na mipango mahususi ya kutatua kero mbalimbali ikiwemo kutekeleza mradi wa maji wa shilingi Bilioni 3 utakaomaliza tatizo la maji katika Jiji la Mbeya.

Kuletwa shilingi Bilioni 18.8 kwa ajili ya kutoa elimu bila malipo, kuletwa shilingi Bilioni 2.137 kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo ya shule, vijiji 580 kupatiwa umeme, vituo vya afya 14 kujengwa kwa thamani ya shilingi Bilioni 6.7 na kupatiwa shilingi Bilioni 14.4za mradi wa uboreshaji wa Jiji la Mbeya.

Mapema kabla ya Mkutano huo Rais Magufuli amefungua jengo la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) lililopo Uzunguni Jiji Mbeya ambalo ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 13 na litatumika kutoa huduma za mfuko huo na kupangisha.

Kesho Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Mbeya ambapo atazindua barabara ya Mbeya – Chunya na ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Chunya – Makongorosi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: