Na Kalunde Jamal, Mwananchi 

Siku chache baada ya Rais John Magufuli kuwataka Watanzania wasiogope kuwa na watoto wengi na waendelee kuzaa huku wakifanya kazi kwa bidii, wadau mbalimbali wameizungumzia kauli hiyo ya mkuu wa nchi.


Rais Magufuli alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na wananchi wa Meatu mkoani Simiyu katika ziara ya kikazi kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Rais aliwaambia wananchi wasiwasikilize wanaowaambia kuhusu njia za uzazi wa mpango na ushauri huo mara nyingi unatolewa na wageni wenye nia mbaya.


Alisema watu wengi wanaofuata uzazi wa mpango ni wavivu kwa sababu wanaogopa kuwa hawataweza kuwalisha watoto wao.


“Hawataki kufanya kazi ngumu kulisha familia kubwa na ndiyo sababu wanaamua kudhibiti uzazi na kuishia kuzaa watoto mmoja au wawili tu,” alisema Rais Magufuli.


“Haya ni maoni yangu, lakini sioni haja yoyote ya kutumia dawa za kujizuia kupata watoto. Nimepita Ulaya na mahali pengine nimeona madhara ya udhibiti wa uzazi. Katika nchi nyingine sasa wanajitahidi kupunguza ongezeko la idadi ya watu, hawana nguvu ya kazi.”


Aliwahimiza Watanzania kuendelea kuzaa kwa sababu Serikali imeongeza uwekezaji katika afya ya uzazi na sekta ya afya kwa ujumla.


Rais alisema Serikali imeanza kujenga hospitali za wilaya 67.


Kiongozi huyo aliyasema hayo mbele ya mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) nchini, Jacqueline Mahon na waziri wa Afya, Ummy Mwalimu.




Kauli ya Rais ilivyogonga


Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe alisema bungeni mjini Dodoma juzi kuwa mifuko ya hifadhi ya jamii inatambua watoto wanne kwa kila familia na iwapo watu wazaana sheria iliyoiunda haitafanya kazi.


“Rais anataka watu wazaliane kadri wanavyoweza, je bima ya afya inalitambua hili?” alihoji.


Alisema iwapo kauli ya Rais itafanyiwa kazi na Watanzania kuna haja ya Mfuko wa Bima ya Afya kuongeza idadi ya watoto inaowatambua kutoka wanne hadi 10.


Akiomba mwongozo wa Spika bungeni Septemba 9, Mwambe alisema uzazi wa mpango wanautambua na wanapokwenda katika bima ya afya, idadi ya watoto wanaogharamiwa na mfuko huo ni wanne pekee.


“Spika naomba mwongozo wako nifahamishwe, kwa nini tunakuwa na Idara ya Umati (Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania) ambayo inasaidia katika masuala ya mpango wa uzazi? Tuongeze idadi ya watoto wanaoweza kutambulika rasmi kisheria kwa sababu hao ndio tunaweza kuwazaa na kuwatunza.”


Akijibu mwongozo huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema huo ni ushauri. Mkurugenzi mtendaji wa Umati, Dk Lugano Daimon alisema kauli ya Rais ina athari kubwa kwao kama wafanyakazi katika taasisi zisizo za kiserikali.


Alisema wanachotakiwa kufanya ni kujitathmini wanatoa elimu ya aina gani kwa wananchi kisha wajipange upya. “Mimi nimemuelewa, wasomi wengi pia watakuwa wamemuelewa kuwa hamaanishi watu wazae tu, anachokipinga ni watu kukatazwa kuzaa kabisa, lakini kama wanazaa kwa mpango hana shida,” alisema Dk Daimon.


Alisema kutokana na kauli hiyo wataandaa mjadala mpana wakishirikiana na wenzao ili kupanga namna ya kutoa elimu ya uzazi wa mpango.


Mkurugenzi huyo alisema ingawa kujua moja kwa moja Rais alikuwa anataka kusema nini ni vigumu, lakini mwelekeo wa kuanzia utapatikana.


Mkurugenzi mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema uhamasishaji wa watu kuzaa unapaswa kwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ikiwamo ya afya.


Alisema watoto wanapokuwa wengi hospitali nazo zitatakiwa kuongezeka, shule, walimu pamoja na makazi kuboreshwa.


“Huduma za kijamii kama vile upatikanaji wa majisafi na salama, wataalamu wa afya, watoa huduma wawepo,” alisema Liundi.


Alisisitiza kuwa, “kuna mahitaji ya familia kama mzazi ajue kabisa ni jukumu lake na hakuna anayeweza kumsaidia mtoto wake kupata elimu bora, kupata huduma za afya na mahali salama pa kuishi.”


“Mzazi akilitambua hilo, ahamasike kuzaa, tofauti na hapo anapaswa kujitafakari kwa kina.”




Wananchi walivyoelewa


Wakizungumza na Mwananchi namna walivyomwelewa Rais Magufuli, baadhi ya wananchi walisema anawahimiza wazae watoto wengi kadri wawezavyo, huku wengine wakionya kauli hiyo inapaswa kutekelezwa baada ya kujitafakari.


Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Mariam Yasini (42) alisema inawezekana Rais alizungumza hivyo akijua wananchi wana elimu ya uzazi wa mpango, lakini kuna haja ya kuwapo mjadala mpana kujadili suala hilo.


“Nimemsikia hata mimi akisema na hii ni mara ya pili anarudia kauli hiyo, ushauri wangu kwa wananchi wenzangu ni kujitafakari kama suala hilo linawezekana kabla ya kuamua kulifanyia kazi,” alisema.


“Serikali kila siku inasema huduma za mama na mtoto ni bure, lakini ukienda hospitali hali ni tofauti.”


Khalid Mussa (46), alisema suala la kuzaa watoto wengi halipaswi kukimbiliwa bila kulitafakari mara mbilimbili.


Alisema kwenye ngazi ya familia ni jukumu la wazazi kuangalia watoto wanaowazaa watawezaje kuwapa mahitaji ya msingi aliyoyataja kuwa ni pamoja na makazi bora na uhakika wa chakula.




Sera ya uzazi wa mpango


Mwaka 1976 Tanzania ilipitisha sera ya uzazi wa mpango ambayo inaeleza hatua mbalimbali za kutumia dawa za uzazi wa mpango ili kudhibiti kuzaana bila mpango na mwaka mmoja baadaye, UNFPA ilifungua ofisi nchini kwa lengo la kuhimiza masuala ya uzazi wa mpango pia.


Sera hiyo ndiyo iliyochangia kuanzishwa kwa taasisi mbalimbali zinazotoa elimu ya uzazi wa mpango pamoja na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayotoa elimu hiyo.

Share To:

Anonymous

Post A Comment: