Kiongozi
wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe jana alijikuta akikwama kumnadi
mgombea udiwani wa Kata ya Turwa wilayani Tarime kupitia Chadema,
Charles Mnanka, baada ya Jeshi la Polisi kumzuia kuhutubia kwa
kuusambaratisha mkutano kwa mabomu ya machozi.
Zitto
ambaye alialikwa kwenye mkutano huo pamoja na viongozi wa Chadema
wakiwa kwenye eneo la tukio, alifika Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tarime
(OCD) na kuwamuru viongozi na wananchi kutawanyika kwa sababu jeshi
hilo halikuwa na taarifa ya kuwapo kwao.
Akizungumza
baada ya kutawanywa mkutano huo na mabomu ya machozi, Zitto
alilalamikia hatua ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya
akisema hatua hiyo ni ukiukwaji wa haki na sheria za uchaguzi.
Alisema
katika tukio hilo, zaidi ya watu 22 akiwamo Mbunge wa Tarime Mjini,
Esther Matiko na mwandishi wa habari, wa Gazeti la Tanzania Daima, Sitta
Tuma, walikamatwa na kushikiliwa katika Kituo cha Polisi.
Zitto
ambaye chama chake kimetangaza kuungana na Chadema katika uchaguzi wa
marudio wa ubunge na udiwani unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka
huu, alisema hatua hiyo ya polisi kuvamia na kutawanya mkutano huo bila
ya taarifa rasmi ni ukiukaji wa Katiba na taratibu za uchaguzi.
“Mkutano
wa hadhara wa kampeni wa sheria kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa
sheria za uchaguzi, upo kwenye ratiba ya kampeni za udiwani za mgombea
wa Chadema kwa mujibu wa katiba na sheria za uchaguzi,” alisema.
Alisema
alifika kuhutubia mkutano huo kwa mwaliko wa viongozi wa Chadema Mkoa
wa Mara kupitia Katibu Wilaya na Mbunge Matiko na akiwa pamoja na
viongozi wa ACT alifika kutimiza wajibu wake akitarajia kushirikiana na
wenyeji wake.
Akisimulia
namna ilivyotokea, Zitto alisema baada ya kufika Tarime, alielezwa na
viongozi wa Chadema mkoa kuwa walipata taarifa za ghafla walizopewa kwa
mdomo kutoka polisi kuwa mikutano yote ya Chadema imezuiliwa kuanzia leo
(jana Agosti 8) hadi Jumamosi Agosti 11 kwa sababu ambazo polisi
wenyewe wanazijua.
Alisema
kwa kuwa huo si utaratibu, waliamua kufanya mkutano kwa kuwa ulikuwa
umeshaandaliwa lakini polisi walivamia na kuuzingira.
Alisema
waliwazuia kuendelea na mkutano huo wazungumzaji waliokuwa
wameandaliwa ambao ni Zitto mweyewe, Mbunge wa Geita (Viti Maalumu
Chadema) Peneza na Matiko (Tarime Mjini Chadema).
Zitto
alilaani kitendo hicho alichodai ni cha uvunjifu wa sheria kwa kuwa
utaratibu uko wazi kwamba iwapo kuna tatizo linalolalamikiwa utaratibu
unaelekeza msimamizi wa uchaguzi.
Alisema
msimamizi wa uchaguzi anatakiwa kuwaita kwa maandishi viongozi wa
kata/jimbo wanaohusika kwenye vikao vya kamati ya maadili, jambo ambalo
halikufanyika, bali walichukua hatua ya kutumia polisi kuvuruga mkutano
huo.
“Kinachoonekana
ni kwamba CCM wameshashindwa katika kata hii, hivyo wameamua kufanya
makusudi kuvuruga uchaguzi kwa kuendesha vitisho kwa kutumia vyombo vya
dola kuwavunja moyo wananchi kushiriki uchaguzi, au kwa kufanya
uchaguzi usiwepo au kuwavuruga wananchi wasijitokeze kupiga kura
wamtangaze wanayemtaka,” alisema.
Alisema
hata baada ya kukamatwa watu 22 waliokuwa kwenye mkutano huo, yeye na
mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza, walifika kituo cha polisi
wanakoshikiliwa kujua kinachoendelea na hali ya mbunge Matiko, katibu
wake na mwandishi anayeshikiliwa, lakini walifukuzwa kituoni hapo.
Alisema
hadi jana jioni walikuwa wakiendelea kuwasiliana na wanasheria na
viongozi wengine kujua hatua wanazoweza kuchukua kutokana na tukio
hilo.
Zitto
aliwataka wananchi wa Tarime watulie wakati wakiendelea kufuatilia na
kuwasiliana na polisi makao makuu kuhakikisha amani haivurugiki na
wananchi wanapewa uhuru na fursa ya kuchagua mgombea wanayemtaka na si
anayetaka kuwekwa na CCM.
Hata
hivyo, muda mfupi baada ya kukamatwa, Sitta ambaye ni mwandishi wa
gazeti la Tanzania Daima aliweza kuandika ujumbe mfupi uliokuwa
ukisomeka “Habari kaka Edwin. nipo Tarime nimekamatwa na polisi nikiwa
natekeleza majukumu yangu ya uandishi wa habari.
“Nimekamatwa
baada ya polisi kuutawanya mkutano wa Chadema wa kampeni kata ya Turwa
Tarime kisha baadaye wakaanza kufyatua mabomu ya machozi. nikiwa napiga
picha tukio la Mbunge wa Tarime mjini Ester Matiko ndiyo polisi
wakanikimbilia na kunikamata”.
Mwandishi
na Mtetezi wa Haki za Binadamu, Edwin Soko, aliandika barua kwa Jeshi
la Polisi kumtambua Tumma ni mwandishi na alikuwa katika eneo hilo
akitekeleza majukumu yake .
“Tuna
imani Jeshi la Polisi lina weledi wa kutambua makosa ya jinai na
taratibu za kushughulikia makosa ya jinai kadri sheria zinavyoelekeza.
“Tuna
imani IGP na RPC wa Tarime/Rorya watalishughulikia suala hili na
mwandishi Tumma ataachiwa aendelee na majukumu yake ya uandishi wa
habari na kulinda uhusiano baina ya Jeshi la Polisi na waandishi wa
habari,’’ ilieleza sehemu ya ujmbe huo kwenda Jeshi la Polisi Tarime
Post A Comment: