Daniel Homa (Chadema) aliyeteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kugombea udiwani kata ya Hayderer wilayani Mbulu mkoani Manyara amejitoa rasmi.

Kufuatia uamuzi huo, mgombea wa CCM, Justin Masuja amepita bila kupingwa.

Kujitoa kwa Homa kumethibitishwa leo Julai 19, 2018 na msimamizi wa uchaguzi jimbo la Mbulu Vijijini, Hudson Kamoga na kubainisha kuwa amepokea barua ya kujitoa kwa mgombea huyo.

“Kwa mamlaka niliyopewa kama msimamizi wa uchaguzi wa eneo hili, namtangaza rasmi mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM, Justin Masuja kuwa diwani mteule anayesubiri kuapishwa baada ya kupita bila kupingwa," amesema Kamoga.

Amesema kwenye kata ya Tumati bado wanasubiri taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya mgombea udiwani wa Chadema,  Zacharia Nihhi kuwekewa pingamizi na mgombea wa CCM.

"Mgombea wa CCM, Paulo Axweso aliweka pingamizi kwa mgombea huyo wa Chadema hivyo tunasubiria majibu kama ataruhusiwa au ataondolewa," amesema.

Akizungumzia kujitoa kwake, Homa amesema amechukua uamuzi huo kwa maendeleo ya Hayderer.

Amebainisha kuwa hajashawishiwa na mtu yoyote kuachia nafasi hiyo, ameamua kumuachia mgombea wa CCM ambaye awali alikuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya Chadema.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: