Na Lilian Lundo – MAELEZO,Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wanaafrika Mashariki kujiamini kuwa wanaweza kutekeleza miradi ya maendeleo bila kutegemea mataifa mengine.

Rais Dkt. Magufuli ameyasema hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa  akihutubia Bunge la Nne la Jumuiya ya Afrika Mashariki linalofanyika mkoani humo kwa mara kwanza  tangu kuanza kwa Bunge hilo.

“Ninazungumza hili si kwamba hatuhitaji msaada au hatuhitaji ushirikiano, lakini ni lazima tuliweke hili wazi, kwamba tukiamua tunaweza na mifano ipo mingi ikiwemo Tanzania”. Alisisitiza Mhe. Rais Dkt. Magufuli.

“Tanzania tunajenga reli ya kisasa yenye urefu wa kilometa 700.26 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa thamani ya shilingi Trilioni 7.6, tumeweza kununua ndege sita na pia tumejenga meli kubwa katika Ziwa Victoria bila kuomba mkopo popote,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ameongeza kuwa wabunge wa Afrika Mashariki wanaowajibu wa kuhakikisha wanalinda na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana ndani ya Jumuiya hiyo.

Akitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana na Jumuiya hiyo Rais Magufuli amesema kuwa kabla ya kuanza kwa umoja wa forodha mwaka 2005 biashara kati ya nchi wanachama ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani bilioni 1.8 lakini baada ya kuanzishwa kwa umoja wa forodha imeongezeka hadi kufikia zaidi ya dola za kimarekani bilioni 5.

Mbali na hayo Rais,  Magufuli ameshukuru uamuzi wa bunge hilo kufanyika mjini Dodoma ambapo kwa sasa Serikali imehamishia shughuli zake zote katika mkoa huo, na tayari watumishi wa serikali zaidi ya 3000 wameshahamia huku Rais Magufuli akitarajiwa kuhamia muda wowote mwaka huu.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Dkt. Martin Ngoga amesema Bunge hilo linasubiri marekebisho ya mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ili  lugha ya Kiswahili ianze kutumika kama lugha rasmi katika vikao vya bunge hilo na katika jumuiya hiyo kwa kuzingatia azimio lililokwishapitishwa.

“Hatuoni sababu ya kutumia lugha za wageni wakati kuna lugha yetu ambayo tunazungumza ambayo ni kiswahili,” alisema Dkt. Ngoga.

Bunge la Afrika Mashariki linaendelea na vikao vyake mkoani Dodoma katika ukumbi mdogo wa Bunge wa Pius Msekwa. Bunge hilo limefanyika kwa mara ya kwanza mkoani humo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: