Serikali imetangaza kutoa zawadi kiasi cha fedha kwa wananchi watakaosaidia kutoa taarifa za siri za kuwafichua watu wanaong’oa alama za barabarani na kuisababishia hasara kutokana na urejeshaji wake.

Ofa hiyo imetangazwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Elias Kwandikwa, baada ya kukagua ukarabati wa eneo la Nyahua ambalo lilikuwa limekatika kutokana na maji ya mvua na kukata mawasiliano kati ya Itigi na Tabora.

“Meneja wa TANROADS nafikiri tuanze kutoa kiasi fulani cha fedha kwa mtu anayetusaidia kutoa taarifa za siri kwa watu wanaong’oa alama za barabarani ili tukomesha tatizo” alisema Naibu Waziri kwenye hotba yake akiwa Nyahua Uyui.

Waziri Kwandikwa amesema lengo la kutoa fedha ni kukomesha vitendo hivyo ambapo Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuweka alama za barabara ili kuepuka ajali kwa watumiaji lakini baadhi ya watu wamekuwa waking’oa alama hizo kwa ajili ya kwenda kuziuza kama vyuma chakavu.

Takribani alama zipatazo 78 zenye thamani ya shilingi milioni 27 katika kipande cha barabara ya urefu wa kilometa zipatazo 80.6 kutoka Tabora hadi Nyahua wilayani Uyui zimeng’olewa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: