Kiingilio cha chini katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa baina ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Jumatatu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kitakuwa Sh. 1,000.
Hayo yamesemwa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo leo mjini Dar es Salaam akizungumzia matayarisho ya mchezo huo.

Ndimbo amesema kwamba kiingilio kingine katika mchezo huo ni Sh. 5,000 kwa majukwaa ya VIP A, B na C na mchezo huo utaanza Saa 10:00 jioni.

Taifa Stars iliyo chini ya kocha Salum Mayanga anayesaidiwa na Hemed Morocco na Patrick Mwangata kocha wa makipa, itaingia kwenye mchezo wa Jumatatu ikitoka kufungwa mabao 4-1 katika mchezo mwingine wa kirafiki na wenyeji, Algeria usiku wa jana Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers.

Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta ataiongoza timu Jumatatu kwenye mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya DRC

Mabao ya Algeria jana yalifungwa na Baghdad Bounedjah mawili dakika ya 12 na 79, Shomari Kapombe moja aliyejifunga dakika ya 45 katika harakati za kuokoa na Carl Medjani dakika ya 53, wakati la Tanzania lilifungwa na Simon Msuva dakika ya 20.

Huo ulikuwa ni mwendelezo wa ubabe wa Algeria kwa Tanzania baada ya Novemba 17, mwaka 2015 The Green kuichapa 7-0 Taifa Stars katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida.

Siku huyo, kiungo Mudathir Yahya alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 41, baada ya njano ya kwanza dakika ya 22 na kipa Ally Mustafa Barthez aliyeanza akafungwa mabao matatu kipindi cha kwanza kabla ya Aishi Manula kuingia kipindi cha pili kufungwa nne naye.

Mabao ya Algeria siku hiyo yalifungwa na Yacine Brahimi dakika ya kwanza, Faouzi Ghoulam mawili dakika ya 23 na 59 kwa penalti, Ryad Mahrez dakika ya 43, Islam Slimani mawili moja kwa penalti dakika ya 49 na lingine dakika ya 75 na Carl Medjani dakika ya 72.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: