KOCHA Mkuu wa Simba, Mfaransa, Pierre Lechantre, tayari ameshakipanga kikosi chake ambacho kitaanza leo Jumatano kwenye mchezo wao dhidi ya Al Masry ya Misri, huku akiwapa jukumu zito la kufunga mabao washambuliaji wake, Emmanuel Okwi na John Bocco.

Mchezo huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa ni wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika na utaanza majira ya saa 12 jioni, ingawa Lechantre hakufura­hishwa na muda huo uliopangwa na viongozi.

Katika mazoezi ya juzi Jumatatu yaliyoanza majira ya saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Boko uliopo jijini Dar, Championi lilimshuhudia Lechantre akipanga kikosi chake kilichoonekana ndicho cha maan­gamizi ambacho kitatumika kum­maliza Mwarabu leo.

Katika kikosi hicho ambacho golini yupo Aishi Manula, walinzi wake ni Shomary Kapombe, Asante Kwasi, Erasto Nyoni, Yusuf Mlipili na James Kotei.

Kwenye kiungo wapo; Jonas Mkude, Nicholaus Gyan, Shiza Kichuya, Bocco na Okwi. Katika ma­zoezi hayo yaliyomalizika saa 1:30 usiku, kocha huyo alikuwa makini zaidi kwenye kushambulia kupitia pembeni.

Aliwapa wachezaji wake haswa wa pembeni namna ya kusham­bulia kwa kasi na kupiga krosi za maana ikiwemo kupiga pasi za mi­pira mirefu huku akiwaeleza kuwa mara nyingi Waarabu hawana kasi lakini wana uhakika na wanachoki­fanya.

Akiwazungumzia wapinzani wao hao, Lechantre alisema: “Tunak­wenda kukutana na moja kati ya timu bora Afrika ambayo inashiriki ligi bora, timu za Misri ni imara, kikweli Al Masry ni timu nzuri na tunaiheshimu.”

“Sitabadilisha mfumo, nitakuwa na washambuliaji wangu wawili, Bocco na Okwi, kwenye kiungo tutaangalia itakavyokuwa pengine nitakuja na ‘sapraizi’ baab kubwa, njooni mkaone.”

Makipa wafanya mazoezi kwa saa matatu
Katika hali ambayo haikutara­jiwa, kabla ya kuanza kwa maz­oezi hayo ya jumla, Championi liliwashuhudia makipa wanne wa kikosi hicho wakianza mazoezi mapema tu kuanzia saa 10:30 jioni wakisimamiwa na kocha wao, Muharami Mohammed.

Makipa hao ni Aishi Manula, Said Mohammed ‘Nduda’, Emmanuel Mseja na Ally Salim, walipoanza muda huo, walikuja kumaliza saa 1:30 sawa na wenzao. ambapo jumla walifanya mazoezi kwa muda wa saa tatu tofauti na siku zote
Share To:

msumbanews

Post A Comment: