Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaaam akizungumza na wananchi wa Kibamba waliokuwa wakionyesha mabango kulalamika kudhulumiwa ardhi yao.
Katika kipindi cha wiki chache zilizopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amepokea mamia ya wageni. Kwa mujibu wa gazeti la The Citizen, watu walifurika kwake wakiamini atawapatia suluhisho la migogoro ya ardhi waliyonayo. RC Paul Makonda ana heshima kubwa aliyojipatia kutokana na kuwasaidia wananchi mbalimbali dhidi ya wananchi wengine wanaowadhulumu. Timu yake kwa kushirikiana na wataalamu wa sheria kutoka Georgia Kemina hutoa msaada wa kisheria kwa watu wa chini.
Mkuu wa Mkoa anafanya jambo jema kwa kuwapa imani wananchi kwamba, matatizo yao yanawezekana kutatuliwa. Lakini inasikitisha kwamba, watu wanaona hakuna haja tena ya kwenda mahakamani kwa mambo ya msingi kama ardhi kwa sababu wanaona haki haitendeki mara nyingi. 
RC Makonda hawezi kufanya jambo hili peke yake, bali ni jukumu la kila mmoja aliyepo madarakani. Juma lililopota, Jaji Mkuu alizungumzia suala la kuhakikisha haki inatolewa kwa kila mtu. Maneno hayo ya Jaji Mkuu yanatoka kwenye kauli za Rais Dkt Magufuli ambaye amenuia tangu mwanzoni kwamba atatokomeza rushwa na kupambana na suala la watu kupata haki zao kwa wakati. 
Lakini utendekaji wa haki, umekuwa ukikwamishwa na rushwa katika ngazi mbalimbali nchini. Hii inamaanisha kwamba kila mmoja anatakiwa kuunga mkono juhudi hizi kuanzia ngazi ya juu hadi chini. Watu wanatakiwa kufichua vitendo vya rushwa, na pia kama vinawaathiri kwa namna yeyote wanatakiwa kusema.
Hatua yetu ya kuanzia inatakiwa kuwashughulikia watu wachache wenye uwezo ambao wanataka kufaidika wao kupitia mali za nchi. Na tusitafute kujidanganya wenyewe, watu hawa tunawafahamu. Mwaka jana Rais aliingilia katika sakata la umiliki wa Coco Beach. Aliweza kumzuia Yusuf Manji pamoja na kampuni yake ya Q-Consult na kuhakikisha kwamba eneo hilo linakuwa wazi kwa ajili ya matumizi ya umma. 
Suala la Ufukwe wa Coco kutosalia mikononi mwa umma linatisha kiasi. Tunashukuru halikufanikiwa, na pongezi ziende kwa wananchi waliopaza sauti zao Rais akawasikia.
Ni kwa sababu hiyo hiyo watu wanafurika kumuona Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Hatutaki watu wachache wenye utajiri wanufaike kupitia ardhi wanayoamini kwamba ni ya kwao huku makabwela wakiwa hawaambulii chochote.
 Hali kama hii ipo katika maeneo yote yenye mgogoro wa umiliki wa ardhi. Nawaunga mkono wafanyabiashara na watu wengine wanaopambana kuweza kuongeza kipato chao na kupata utajiri, lakini njia wanazotumia zinapaswa kuwa halali.
Rais na viongozi wengine kama RC Paul Makonda wapo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi, lakini wanahitaji msaada wetu kufanikisha hili kwani kuna wengine zaidi ya maelfu ambao hawajasikika bado katika nchi yetu. Tunaowaona wanafurika kwa Makonda ni wa Dar tu, ila tukumbuke tuna mikoa mingine Zaidi ya 25. 
Tunapaswa kuwashughulikia wale wote wanaopata utajiri wao kwa njia ya udanganyifu na dhuluma. Uhalali wa serikali ni uwezo wake wa kupinga dhuluma dhidi ya wanyonge. Tunapaswa kupaza sauti zetu tukipinga vikali vitendo vya rushwa.

Share To:

Post A Comment: