Klabu ya soka ya Azam FC imesema imejiandaa vyema kuhakikisha inashinda mchezo wake wa leo dhidi ya Simba ili kuendelea kuikimbiza timu hiyo katika mbio za ubingwa kwakuwa wao ndio vinara.

Msemaji wa timu hiyo Jaffary Idd amesema kocha wa timu hiyo Aristica Cioaba ameandaa kikosi chake vizuri kwasababu wanaamini ushindi wa aina yoyote leo utawaweka katika mazingira mazuri ya kusaka ubingwa.

''Ushindi wowote kwa Azam leo maana yake tutakuwa tunamkimbiza kimya kimya kinara wa ligi na yoyote aliyepo juu kwenye msimamo'', amesema.

Aidha kwa upande mwingine Jaffary amesema kuwa wachezaji waliokuwa majeruhi akiwemo nahodha Himid Mao tayari wamepona na kujiunga na timu isipokuwa wawili tu ambao ni Waziri Junior pamoja na Joseph Kimwaga.

Azam FC kwasasa inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 31 nyuma ya Yanga yenye alama 34 na vinara Simba wenye alama 38. Mchezo wa leo utachezwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.
Share To:

Post A Comment: