ZAHANATI mbili zimefungwa kwa kukosa watumishi wa kada ya afya katika Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma na kupelekea wananchi kusafi ri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Hayo yalibainika juzi wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge kwa lengo la kukagua shughuli mbalimbali za maendeleo. Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Dk Olden Ngassa alisema wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya nchini zenye upungufu mkubwa wa watumishi wa kada za afya wakiwemo madaktari na wauguzi ambapo kati ya watumishi 632 wanaotakiwa, waliopo ni 142.


Alivitaja zahanati zilizofungwa kwa kukosa watumishi ni Chase na Igunga. Alisema wilaya hiyo yenye kata 26 na vijiji 114, ina zahanati 31 ambazo mbili zilifungwa kutokana na uhaba wa watumishi na kuna vituo vya afya vinne.


Dk Ngassa alisema upungufu huo mkubwa unatokana na uchache wa watumishi kada ya afya ili mwananchi apate huduma makini. Alisema kuna uhaba mkubwa wa watumishi wa kada ya unesi na waganga na vituo vingi vinaongozwa na wahudumu wa afya na hakuna zahanati yenye watumishi zaidi ya wawili.


Alisema kama kituo kina mtumishi mmoja basi hulazimika kufanya kazi saa 24 pasipo kupumzika. Alisema wamefanya mikakati mbalimbali ili kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kuwasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma na sasa jitihada zinafanyika na tayari wameletewa watumishi 12, lakini mpaka sasa hawajaanza kazi kutokana na taratibu zao za mishahara kushughulikiwa.


Pia alisema wilaya hiyo haina hospitali ya wilaya, lakini mchakato wa kupata hospitali umeanza na ekari 27 zimetengwa kwa ajili ya kujenga hospitali ya wilaya. Katibu Tawala wa Mkoa, Rehema Madenge alisema tatizo la watumishi wenye vyeti feki lilichangia kwa kiasi kikubwa kupunguza watumishi kwenye kada ya afya.


Alisema changamoto hiyo wameiona na wanaifanyia kazi. Mkuu wa mkoa, Dk Binilith Mahenge alisema suala hilo linafanyiwa kazi kwani hali si nzuri.


Share To:

msumbanews

Post A Comment: