BAADHI ya wakazi wa Mtaa wa Matarawe katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamekusanyika katika eneo la viwanja vya Shule ya Msingi Kipika mjini hapa na kudai warudishiwe michango yao ya fedha walizochangishwa kuanzia mwezi huu.Wiki hii, Rais John Magufuli alitoa tamko kupiga marufuku michango kwa shule za msingi na sekondari nchini, akisisitiza kwamba yeyote anayekiuka agizo hilo anapaswa kuchukuliwa hatua kali.

Juzi asubuhi, wakazi wa Mtaa wa Matarawe ambao ni wazazi wenye watoto wanaosoma shuleni Kipika, walikusanyika baada ya diwani wa kata hiyo, Leonard Mshunju kuitisha mkutano wa dharura ili kujua hatma ya michango ya fedha, mahindi na maharage walivyochangishwa kwa chakula cha watoto wanaosoma shuleni hapo.

Baada ya ufunguzi wa mkutano huo, wazazi hao walisema hawawezi kupingana na tamko lililotolewa na Rais Magufuli kwani wakati wanachangishwa michango hiyo baadhi yao walikuwa wakipewa vitisho huku wengine watoto wao wakikosa nafasi ya kuandikishwa kuanza shule darasa la awali kutokana na kukosa mchango husika.

Naye Diwani wa Kata ya Matarawe, Mshunju aliwataka wazazi hao watulie na kueleza kuwa lengo la mkutano huo ni kutaka kufikia muafaka juu ya michango yao waliyochangishwa ya chakula na fedha warudishiwe au la.

Pamoja na mambo mengine, baada ya mvutano wa muda mrefu wazazi hao walifikia muafaka kwamba watarejeshewa michango yao waliyochangia ifikapo kesho wakaichukue shuleni hapo.

Aidha mwandishi wetu amebaini  pamoja na wazazi hao kuchangishwa michango, hapakuwa na risiti yoyote na michango hiyo ilianza kukusanywa Novemba 30, 2017 na mwisho ilikuwa ni Januari 8, mwaka huu.

Ukusanyaji wa michango hiyo ulikuwa ukifanyika kwa mwaka mzima, watoto kuanzia darasa la awali walikuwa wakichangia Sh 10,000 darasa la kwanza, la pili mpaka la saba Sh 5,000 pamoja na dumu mbili za mahindi na maharage.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: