Na Oscar Assenga, TANGA
SERIKALI imesema kwamba ina mpango wa kuendelea kufanya uwekezaji katika Bandari ya Tanga kwa kuongeza sehemu ya kutoa huduma mara mbili kutoka mita 450 hadi kufikia mita 900 ili kuendelea kuongeza ufanisi wa kuhudumia shehena
Hayo yalibainishwa Septemba 1,2025 na Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu wakati alipofanya ziara katika Bandari ya Tanga kuona uwekezaji uliofanywa na Serikali wa Sh.Bilioni 429.1, huku akiridhishwa na maboresho yaliyofanyika ambayo yameiwezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Alisema kwamba uwekezaji katika Bandari hiyo utaendelea kuwa chachu ya kuongeza matokeo ya wazi ya kiuchumi kutokana na kuchangia uwepo wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na hivyo kuchangia maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla.
Aidha alisema kwamba katika sehemu ya kutolea huduma kuna mita 450 na kina mita 3 na kinaenda kuwa mita 13 ikiwemo lango la kuingilia limepanuliwa na kufikia upana mita 135 kwa kina cha mita 13 lakini bado kuna mipango inafanyika kuongeza ifike mita 900.
“Tunaiona Bandari hii ikichangamka tayari Serikali inakwenda kufanya uwekezaji mara mbili kutoka mita 450 mpaka mita 900 maana yake ni mita ni 1800 sasa unapokuwa unaangalia maeneo ya Bandari uwekezaji huo na ule uwekezaji wa Chongoleni kwa ajili ya mafuta ukiangalia gati inayotengenezwa kwa ajili ya Meli kubwa zinazokuja kusafirisha mafuta ghafi yanayotoka nchini Uganda huu ni uwekezaji mkubwa ”Alisema
Aliongeza kwamba maana tayari eneo la Tanga litakuwa ni kitovu cha biashara pamoja na eneo ambalo kila mtu kutoka mataifa mbalimbali atakuwa anaifahamu na kuwa na uwekezaji mkubwa na kuleta nafasi kubwa za kiuchumi sio kwa mkoa bali nchi nzima.
“Kimsingi mimi kama Msimamizi wa Mashirika na Mmiliki kwa niaba ya Serikali ninafarijika na huduma zinazotolewa na TPA na utulivu tunauona uimara wa huduma maana yake ni muunganiko wa vitu viwili uongozi inayofahamu kazi yake na watumishi wanaofanya kazi yao kwa ustawi wa juu”Alisema
Alisema kwamba wanazidi kuwa na matumaini makubwa sana kwa sababu Bandari asilimia kubwa ya mapato yake yanayokusanywa na TRA wanatoka Bandari na wanafikiria ni muhimu kuendelea kuitazama Bandari kwa jicho la Pekee.
“Lakini niwasihi wafanyakazi wa Bandari tuone ufahari tupo sehemu ambayo ni jicho na mboni ya Serikali katika uchumi wa nchi kwa hivyo lazima tuichukulie kama sehemu muhimu inayohitaji huduma zilizobora na tija kwa ajili ya maendeleo”Alisema
Hata hivyo alisema kwamba jambo jingine ni kuendelea kuhakikisha sekta binafsi na umma zinaungana lakini mali inabaki kuwa ni ya Bandari na zitabali kuwa mali ya nchi na wananchi kwa ujumla.
“Tunachokizungumza hapo ni na wanachokizungumza ni wawekezaji ambao watakuja kuziendesha na watapata mapato lakini baada ya muda kile kitu ni mali yetu na hakiondoki na maana yake tunakuwa na ushindani na ufanisi na huduma zitaendelea kuwa bora hivyo ni jambo la msingi na watanzania waendelea kujiunga na kujifunza kwa waliokuja kuwekeza”Alisema
Awali akizungumza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Plasduce Mbossa alisema uwekezaji wa viwanda huo umesaidia kuhudumia meli kwa urahisi na gharama nafuu kutokana na kuimarika miundombinu ya Bandari ya Tanga
“Sisi tumekusanya Bilioni 75 ambazo tunatumia kulipa wafanyakazi,vifaa na kufanya ukarabati tunatumia fedha hizo Tanga kuna ukuaji mkubwa wa viwanda na kichosabababisha ni Bandari sasa tunaweza kuhudumia meli kwa urahisi na bei nafuu ndio inapeleka uwekezaji wa viwanda”Alisema
Hata hivyo alisema ujenzi viwanda vilivyo vinasababisha ukuaji wake kuimarika kwa Bandari ikiwemo maboresho walioyafanya na ukuaji wa uchumi na mahitaji na maendeleo yanazidi kufanywa ikiwemo upanuzi zaidi na watajenga mita 900 zaidi.
“ Leo utaona kuna meli mbili zinahudumiwa na meli tatu nje zinasubiri hivyo tunahitaji kupanua miundombinu ili kuweza kuzihudumia meli zote kwa wakati na kuwasaidia wafanyabiashara na wakulima kulifikia soko kupitia Bandari ya Tanga”Alisema
Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha alimhakikishia Msajili huyo kuwa huduma katika Bandari ya tanga itazidi kuimarika kwa maana ya kwamba meli zitakapokuwa zinakuja watazihudumia sio kwa zaidi ya siku tatu meli inaondoka huku akitoa wito kwa watumiaji wa Bandari hiyo waendelee kuitumia