Saturday, 6 June 2020

MKUU WA WILAYA YA MONDULI AIPONGEZA ALAT MKOA WA ARUSHAMkuu wa wilaya ya Monduli Ameipongeza ALAT Mkoa wa Arusha kwa usimamizi mzuri  katika kusimamia Halmashauri zote katika mkoa wa Arusha kwani  kumekuwa na utekelezaji Mkubwa katika Miradi ya Maendeleo katika  Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha.
.
.
.
Mkuu wa wilaya Monduli  amesema hayo alipokuwa akihutubia Kikao cha Mwisho cha ALAT ambapo wanahitimisha Miaka mitano katika kusimamia Halmashauri zote katika kutekeleza majukumu  Mbalimbali.


Dc Kimanta   amewapongeza Waheshimiwa Madiwani ambao ni wajumbe wa Kamati ya ALAT kwa kuondoa  tofauti zao na  kuweka Maslahi mbele  ya kuwahudumia wananchi na kwakuwaletea  maendeleo.Amewatakia  Heri huko waendako na kuwataka Watembee kifua mbele kwani wamefanya kazi kubwa Ambazo zinaonekana katika Usimamizi wa Halmashauri na Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji Wa   Halmashauri ya wilaya ya Monduli Ndg.Stephen Ulaya amesema wamepata mafanikio makubwa na ikiwemo usimamizi mzuri katika miradi na Kusimamia pia Stahiki za Madiwani na kipindi hiki wao kama watendaji wataendelea  kusimamia yale yote yameadhimiwa katika kikao hicho  ambapo yanatakiwa kufanyiwa utekelezaji.

RC MAKONDA AWAELEKEZA POLISI KUWASHUGHULIKIA KIKAMILIFU VIBAKA NA WANAOPORA MALI ZA WATU


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda amemuelekeza Kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam kuhakikisha wanawashughulikia ipasavyo baadhi ya vijana walioanza tabia ya kupora na kuiba Mali za Watu jambo linalorudisha nyuma maendeleo ya Watu.

RC Makonda amesema operesheni maalumu ya kushughulikia Vibaka hao imeanza rasmi jana ambapo amemtaka kila mzazi kuhakikisha anamchunga mwanae kwakuwa hakuna kibaka atakaesalimika katika msako huo.

Mhe. Makonda ametoa agizo hilo wakati wa Ziara ya ukaguzi miradi ya maendeleo Wilaya ya Temeke iliyoenda sambamba na uzinduzi wa Majengo ya Madarasa 124, Matundu 124 ya Vyoo na Madawati 7,179 kwenye Shule ya Sekondari Mbagala na Shule nyingine 16 Wilayani humo jambo linalokwenda kusaidia zaidi ya Wanafunzi 5,000 waliofaulu na kukosa nafasi kupata uhakika wa kuendelea na masomo.

Aidha RC Makonda ametembelea Ujenzi wa kituo cha Afya Buza na Hospital ya Yombo Vituka yenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa 2,000 kwa Siku ambapo amesema kuongezeka kwa Zahanati, Vituo vya Afya na Hospital vinakwenda kurahisisha upatikanaji wa Huduma za Afya kwa wananchi.

Pamoja na hayo RC Makonda amesema ifikapo Juni 20 ataanza Ziara ya Siku 10 na Kamati ya Siasa ya Mkoa kwenye kila jimbo kwa lengo la kukabidhi miradi iliyokamilika ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Vitendo.

Katika Ziara hiyo RC Makonda pia ametembelea Ujenzi Mitaro yenye urefu wa Km 9 Wilayani humo ikiwemo mtaro mkubwa kabisa unaojengwa eneo la Serengeti kuelekea Shule ya Sekondari Kibasila na Maradi na Mradi wa uwezeshaji wa vijana kupitia 10% ya mikopo inayotolewa kwenye halmashauri ambapo ameipongeza Manispaa hiyo kwa namna inasimamia miradi ya maendeleo.

Friday, 5 June 2020

JUMUIYA YA WAZAZI MAKURUMLA YATUMIA WIKI YA MAZINGIRA KUSAFISHA MAKABURI


 Wanachama wa CCM,wa kata ya Makurumla,  wakisafisha makaburi ya Mburahati Dar es Salaam katika maadhimisho ya wiki ya mazingira

FARAJA MASINDE

-DAR ES SALAAM

WAKATI Wiki ya mazingira duniani ikifikia ukingoni Umoja wa Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Kata ya Magomeni Makurumla umetumia wiki hiyo kuwakumbuka waliotangulia mbele za haki kwa kusafisha makaburi.

Akizungumza na leo wakati wa zoezi hilo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Kata ya Magomeni Makurumla, Shukuru Abdalla amesema lengo la kusafisha makaburi hayo ya Mburahati nikutokana na umuhimu wake pamoja na ukaribu wa kituo cha Afya kilichopo hapo.

Amesema zoezi hilo halitaishia leo badala yake litakuwa endelevu katika kuhakikisha kuwa makaburi hayo yanasafishwa na kuwa salama.

“Tumekuja katika eneo hili la makaburi sababu tuko kwenye maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani na sisi tumeamua kutumia siku hii kwa kufyeka na kufanya usafi katika makaburi yetu ya Mburahati kwani sisi sote tunajua ni wafu watarajiwa na hapo walipolala Wazee wetu, Mama zetu, Dada zetu na Kaka zetu ndipo tumeona ni sehemu muhimu ya kufanyia usafi kwasababu hili ni eneo muhimu sana.

“Ukiondoa eneo la makaburi, hapa pia kuna kituo cha Afya cha Makurumla hivyo majani yakiwa mengi yanaweza kuogopesha hata Manesi na Mdaktari kufika kazini hasa nyakati za usiku sababu yanaweza kuficha vibaka na watu wasiokuwa na nia njema,” amesema Abdallah.

Amefafanua kuwa, hiyo imekuwa ni kawaida ya Umoja huo katika kufanya usafi kwenye wiki ya mazingira duniani ambapo wamekuwa kifanya usafi katika kituo cha Afya, huku akisisitiza kuwa wanampango wa kuwaarifu wananchi wote kushiriki kwenye usafi wa makaburi hayo.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kukiunga mkono chama cha mapinduzi kwa kuwa mietekeleza mambo mengi makubwa ndani ya miaka mitano chini ya Rais Dk. John Magufuli.

“Wito wangu kwa Watanzania huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo wampigie kura Rais Magufuli kwani mengi tumeyaona, sasahivi hata ukitoka mkoani ukifika Ubungo pale utaona mambadiliko makubwa ukiondoa hilo ameongeza dawa katika vituo vya afya na hospitali bado anajenga mradi wa bwawa la kufua umeme la Nyerere litakalopunguza gharama za umeme kwa wananchi na mambo mengine mengi,” amese Abdalla.

Upande wake Diwani wa Viti Maalum Halmashauri ya Ubungo, kutoka Kata ya Makurumla, Rehema Mayunga, amesema wamechagua kufanya usafi wa makaburi hayo kwa kuwa ndiyo sehemu wanayoishi na kwamba wananchi wengi wamekuwa kihifadhiwa katika eneo hilo huku akimshukuru Rais Magufuli kwa namna alivyopambana na janga la corona.

“Tumefanya hivi kuwakumbuka wapendwa wetu katika kuhakikisha kuwa wanalala sehemu nzuri ikizingatiwa kuwa hii ni wiki ya mazingira. Pia niwatake wananchi hususan wanawake wenzangu kuchagua viongozi wanaoweza kuwaletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kutatu changamoto zao, mfano mzuri ni Rais wetu ambaye nibayana kwamba ameweza kutuvusha katika mambo mengi ikiwamo janga la corona,” amesema Rehema.

Naye Katibu wa CCM kata ya Makurumla, Salama Mlaponi, amefafanua kuwa, wamechagua kufanya usafi kwenye eneo hilo la makaburi kwa kuwa wote ni marehemu watarajiwa ikiwamo kuweka mazingira safi.

“Hapa pia kuna kituo chetu cha afya hivyo tuliona ni jambo la busara kuweka mazingira mazuri hapa kwani kichaka hiki likuwa kikitishia usalama, sababu iliwahi kukutwa maiti ya kijana hivyo tunaona ni jambo la busara kuweka mazingira safi.

“Pia kuelekea katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu ushindi kwa CCM Kata ya Makurumla ni lazima na tumejipanga vyema kwenye hilo kuhakikisha kuwa kata hii inakuwa chini ya CCM,” amesema Salama.

Akizungumzia zoezi hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwajongo, Omar Omary amesema Jumuiya hiyo ya Wazazi imeamua kufanya hivyo ili kuweka salama makazi ya wapendwa wao na kupata fadhila za Mwenyezi Mungu.

“Nahimiza pia jumuiya nyingine kuiga utaratibu huu ikiwamo Umoja wa Vijana, Umoja wa Wanawake kuendeleza msukumo huu wa kuhudumia jamii,” amebainisha Omary.

RC Mgwira aagiza kuondolewa mtandaoni video za waliofumaniana.


Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt Anna Mghwira ameagiza kuondolewa mtandaoni video zenye viashiria vya udhalilishaji kwenye mahojiano ya Wanandoa Agnes Mushi na Mumewe Vicent Malya wanaotajwa kuhusika na shambulio la mwili wa Vena Kimario baada ya kufumaniwa kwa kile kinachoelezwa kukiuka maadili na kuwadhalilisha wanawake.

Tuwe wajanja tusije tukafa kwa kukosa maarifa, mtu akikupa barakoa kataa mwambie akavae na mkewe- JPM


"Watu watakuja Kuwaambia Mvae, Watanzania tujifunze kuelewa. Anapokuletea Mtu Barakoa na haujui hata ameitoa wapi kataa mwambie akavae yeye na mke wake na watoto wake Nyumbani kwake TUTAUMIZWA

Tuwe wajanja tusije tukafa kwa kukosa maarifa" - Rais MAGUFULI

“Ukitaka kuvaa barakoa kashone yako, mbona ni rahisi tu, barakoa mbona imekaa kama titi moja la Mtu mmoja hivi limekatwa upande mmoja, weka huku kama... aaah samahani Mh.Waziri nimesema hapa, nilikuwa nachomekea tu kidogo” -JPM

“Juzi nilikuwa nasikiliza taarifa ya habari kuna group linaitwa Magufuli Forum wala silijui, ila sishangai Mtu kujiita Magufuli hata akijiita fisi ni hiyari yake, lakini walikuwa wanagawa barakoa wala hazijulikani zinatoka wapi, tutaumia kwa kukosa maarifa”-JPM

WAZAZI MBARALI WAASWA KUTOIPUUZA CORONA KUWALINDA WATOTO.

Na Joachim Nyambo,Mbarali.
WAKAZI wilayani Mbarali mkoani Mbeya wametakiwa kutobweteka na badala yake watambue kuwa bado wanapaswa kuendelea kuchukua tahadhali na kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa kufuata taratibu zote zilinazotolewa na Viongozi Wakuu wa Nchi pamoja na Wizara ya Afya.
Tahadhari zaidi imetakiwa kuimarishwa majumbani hasa wazai wanaporejea wakitokea kwenye mizunguko ya utafutaji ambapo hukutana na watoto wakiwamo wadogo wasiotambua umuhimu wa kuchukua tahadhari na mara nyingi hulazimisha kukutana kwa haraka na wazazi wao kwa kuwalaki hata kabla hawajafuata kanuni za kujikinga ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali,Reuben Mfune, kwa sasa wilayani hapa kuna baadhi ya maeneo watu wanaonekana kuanza kujisahau na wameacha kuendelea kuchukua tahadhari.
Mfune aliyasema hayo alipokuwa akifungua warsha iliyoandaliwa na Mtandao wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoani Mbeya(Mbengonet) iliyolenga Kujenga uwezo kwa jamii na kuimarisha mifumo ya Serikali ili kupunguza kasi ya ongezeko la maambukizi ya COVID-19 na kuleta Mabadiliko chanya dhidi ya mila, desturi na tabia zinazochangia maambukizi katika mkoa wa Mbeya.
Mkuu huyo wa wilaya alisema bado ni mapema sana kuamini kuwa maambukizi ya Corona hayapo kabisa na jamii kurudi katika maisha yaliyokuwa yamezoeleka bali lazima tahadhali zinendelee kuchukuliwa kwa kufuata miongozi iliyowekwa.
Sambamba na tahadhali kwa wananchi,alisema bado jitihada za wadau zinahitajika katika kuisaidia Serikali kuendelea kutoa elimu ya kujikinga na Corona na kuupongeza mtandao huo kwa kuwa sehemu ya wadau waliamua kujitoa katika utoaji elimu ndani ya jamii.
Mfune aliutaka mtandao wa Mbengonet kufika maeneo yote yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama miji midogo iliyopo barabara kuu ya TANZAM lakini akasihi watakapokuwa wanatoa elimu hiyo wasiwajengee hofu wananchi, ila wawape ujumbe na kuwaelekeza kuendelea kujikinga na kuchukua tahadhari sambamba na kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuinua vipato vyao na uchumi wa nchi.
“Watu wengi wanatafsiri vibaya kauli ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.Rais Magufuli hajasema Corona imeisha Tanzania, ila kasema Corona imepungua kwa kiasi kikubwa nchini kwetu. Kuna baadhi ya watu kwenye jamii wanapuuza taratibu za afya zilizowekwa ili kupunguza uwezekeano wa kuenea kwa ugonjwa huu hasa katika sehemu zenye mikusanyiko.”

“Siku hizi tunajikinga na Corona tunapotoka nyumbani kwenda kwenye mihangaiko yetu, ila tunasahau kuzikinga familia zetu pale tunaporudi nyumbani, ni vyema kila mtu akachukua tahadhari kwa kuweka ndoo yenye maji tiririka na sabuni nyumbani kwake.” Alisema Mfune

"Utakuta pale nyumbani watoto wadogo na hivi kwa sasa hawaendi shuleni wameshinda hawakuoni baba au mama sasa unaporudi wao hawajui kama kuna Corona wanataka moja kwa moja ukae nao uwanyenyue kwakuwa ndiyo furaha kwao.Hapo tunapaswa kuwa makini kunawa kwanza."aliongeza

Awali Katibu Mtendaji wa Mtandao wa Mbengonet, Paul Kita alisema kuwa Shirika limejipanga kwenda kutoa elimu ya kujikinga na COVID- 19 na kuhamasisha matumizi ya Barakoa na vitakasa mikono kwa waendesha Bodaboda, Madereva wa Bajaji, kwenye minada pamoja na kwenye Mikusanyiko kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Serikalini.

Kita aliongeza kuwa baadhi ya watu katika jamii wameanza kukusanyika kwenye baadhi ya maeneo bila kuchukua tahadhari na wamegundua baadhi ya maeneo mengi ni machafu kitu ambacho kitasababisha magonjwa mengine ya mlipuko kwani kinachoua watu kwa sasa sio Corona pekee hata uchafu na magonjwa mengine

Mbengonet ni mtandao ambao umekuwa na mchango mkubwa mkoani Mbeya katika Uelemishaji, Uhamasishaji na Ushawishi wa shughuli za maendeleo katika sekta za Afya, Kilimo, Maji, Elimu, Utawala bora pamoja na Haki za binadamu.

Halmashauri ya wilaya ya Babati yaomba kupatiwa Magari ya kubebawagonjwa,Kuongezewa watumishi.

Na John Walter-Babati
Halmashauri ya wilaya ya Babati  mkoa wa Manyara, imeomba kupatiwa msaasa wa  gari la wagonjwa ili kuweza kukabiliana na changamoto inayowakabili ya kusafirisha wagonjwa.
Ombi hilo limetolewa na Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Babati  Dr.Hosea Madama  akitoa taarifa ya idara ya afya kwa Naibu waziri wa TAMISEMI Josephat Kandege wakati wa uzinduzi wa Zahanati ya Kijiji cha Gajal kata ya Ayalagaya.
Dr. Madama amesema kuwa wapo katika njia kuu na ajali nyingi hutokea hivyo serikali na wadau mbalimbali wajitokeze kusaidia kupatikana kwa  magari hayo kwa vituo vya afya saba vilivyopo ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Babati.
Aidha Dr.Madama ameomba serikali  kutoa fedha za kujenga miundo mbinu inayohitajika katika zahanati mbili za Dareda Kati na Bashnet zilizopo katika tarafa ya Bashnet ili kusaidia kutoa huduma za dharura na upasuaji kwa wananchi.
Amesema licha ya Halmashauri hiyo kuwa na hospitali mbili,  Zahanati 40 nyingi zikiwa ni za serikali pamoja na vituo vya afya saba, lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za upungufu wa nyumba za watumishi pamoja na watumishi wa kada hiyo.
Ameeleza kuwa Idara ya watumishi wa afya ina jumla ya watumishi 324 ambapo  wanaohitajika ni 747 sawa na asilimia 43, huku nyumba za watumishi zikiwa 14 wakati hitaji ni nyumba 84  sawa na asilimia 16 ya hitaji.

Kuboreshwa kwa huduma za afya katika Halmashauri ya wilaya ya Babati,  itawasaidia wananchi wa wilaya hiyo wanaokadiriwa kuwa zaidi ya laki tatu (300,000)  ikiwa na Tarafa nne (4) , kata 25, na vijiji mia moja na mbili (102)
Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Mheshimiwa Jituson Vrajilal ameiomba serikali pindi inaposambaza vifaa katika vituo mbalimbali, ikumbuke kituo cha Dareda kati.
Mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu  amesema wamepokea fedha za kutosha katika kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwepo za ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Babati vijijini ambayo haikuwepo.
Naye  Naibu waziri ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Josephat Kandege  akizindua zahanati hiyo iliyogaharimu jumla ya shilingi Milioni 245,595,000, amewapongeza wananchi wa kijiiji cha Gajal na uongozi wa kijiji  hicho kwa kujitolea na kuanzisha ujenzi wa jengo la Zahanati  hiyo.

MEYA TANGA ATAKA HALMASHAURI IWEKWE KWENYE REKODI KWA KUPATA HATI SAFI MIAKA MITATU MFULULIZO

 MSTAHIKI Meya wa Jiji la Tanga Alhaj Mustapha Selebosi akizungumza wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani ambacho kilikuwa kikao maalumu cha kupitia na kujadili hoja za mkaguzi na mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG)kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella na kulia ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji
 MKUU wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella akizungumza wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani ambacho kilikuwa kikao maalumu cha kupitia na kujadili hoja za mkaguzi na mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG)kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Judica Omari na kulia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Alhaj Mustapha Selebosi
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Judica Omari akizungumza wakati wa kikao hicho
 Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daudi Mayeji akizungumza wakati wa kikao hicho
 Sehemu ya madiwani wa kata mbalimbali wakifuatilia kikao hicho
 Maafisa kutoka ngazi ya Mkoa wa Tanga wakifuatilia kikao hicho kulia ni Afisa wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Tanga Gipson George
 Sehemu ya wataalamu wa Halmashauri ya Jiji la Tanga wakifuatilia kikao hichoMSTAHIKI Meya wa Jiji la Tanga Alhaj Mustapha Selebosi amesema ni muhimu Halmashauri ya Jiji hilo iandike kwenye historia kutokanana na kupata hati safi ya mahesabu miaka mitatu mfululizo huku akieleza hilo limewewezeshwa na mshikamano uliopo katika ufanisi wa kazi .

Huku akieleza hilo limefanikishwa na watendaji wa Halmashauri ya Jiji wakiongozwa na Mkurugenzi Daudi Mayeji ambao wamekuwa wakipambana kuhakikisha mafanikio hayo yanapatikana.

Aliyasema hayo wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani ambacho kilikuwa kikao maalumu cha kupitia na kujadili hoja za mkaguzi na mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ambapo alimueleza Mkuu wa Mkoa wa Tanga kumfikishia salamu zao Rais Dkt John Magufuli kwa kuitendea haki Halmashauri hiyo kwenye miradi mbalimbali.

“Kwa hili tunafarijika sana kwani Jiji letu limeandika historia kubwa ya kuendelea kupata hati safi mpaka leo hivyo nadhani ingekuwa ni vizuri ingeeandikwa kwenye vitabu ambapo kesho na kesho kutwa watu watambue kwamba viongozi hao walifanya kitu gani”Alisema

Meya huyo alisema kwamba mabaraza yaliyopita walikuwa madiwani tisa wa upinzani lakini mabaraza yalikuwa hayaendi vizuri katika vikao vya halmashauri lakini kwa sasa walikuwepo 20 wa upinzani na 17 wa CCM lakini kwa kuheshimiana wamefanya kazi pamoja bila kujali itikadi za vyama.

“Wakati tunaanza baraza letu tulikuwa na madiwani 20 wa upinzania na 17 CCM lakini kwa kuheshimiana tumefanya kazi pamoja bila kujali itikadi za vyama kwa lengo la kuitanguliza tanga mbele kuheshimiana pekee bali ni utulivu wa Mkurugenzi wa Jiji Daudi Mayeji na Wetandaji wake na hii ni historia haijawahi kuandikwa “Alisema

Hata hivyo Meya huyo alimpongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga (CCM) Ummy Mwalimu kwa kuwa kiunganishi kikubwa cha maendeleo kwenye Halmashauri hiyo kwa kuwasilisha kero zinazowakabili na hivyo kupatiwa ufumbuzi haraka.

“Kwa kweli Waziri Ummy amekuwa msaada mkubwa sana kwetu kwani kabla hajaingia bungeni anakupigia simu anaachukua taarifa za halmashauri na hivyo hatua hiyo imekuwa chachu kubwa kwa maendeleo ya Jiji hilo na sisi kama tutaendelea kushirikiana naye na kumsapoti”Alisema Meya.

Awali akizungumza wakati wa kikao hicho Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Judica Omari alisema kwamba makusanyo ya Halamshauri hiyo kuwa asilimia 76 sio mbaya lakini wanatakiwa kujitahidi vyanzo ambavyo vimeorodheshwa hapo ni vingi na vile ambavyo vimepitishwa karibuni wavisimamie kwa ukaribu.

Alisema huo ushuru wa madini,taka ngumu ,nyumba za kulala wageni ikiwemo mazao mbalimbali na mifugo vyote wavisimamie kwa karibu kwa wakati kuhakikisha wanakusanya kodi ili kuweza kutimiza malengo yao na la pili ni upande wa kuangalia mapato bado yapo mikononi mwa wakusanyaji ambayo bado hayajaingia kwenye mfumo na benki .

Hata hivyo aliwaomba wasimamie na kuweka muda maalumu ili fedha ziilingizwe kwenye akaunti na zinaweza kuongeza mapato ya JijiKwa upande wake MKUU wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kupata hati safi na hilo linatokana na usimamizi imara ambao umekuwa mfano wa kuigwa katika maeneo mengine.

Mwisho.

BODI YA MAZIWA NA WADAU KUWEKA MIKAKATI YA KUZALISHA MAZIWA YA KUTOSHA NCHINI


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina akizungumza na wandishi wa habari na wadau wa maziwa wakati wa kilele cha wiki ya maziwa jijini Dodoma.
Sehemu ya Wadau wa maziwa wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina wakati wa kujadili mambo mbalimbali ya sekta ya maziwa katika wiki ya maziwa ambayo kitaifa imefanyika jijini Dodoma.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe Patrobas Katambi,aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma akizungumza na wadau wa maziwa wakati wa kilele cha wiki ya maziwa jijini Dodoma.
Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote akizungumza na wadau wa bodi ya maziwa wakati wa ufungaji wa kilele cha siku wiki ya maziwa.
Mwenyekiti wa Baraza la wadau ni Bi.Catherine Dangat,akizungumza na wadau wa maziwa wakati wa kilele cha wiki ya maziwa jijini Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (wa pili kushoto) akinywa maziwa kuashiria kufunga wiki ya maziwa nchini sambamba na Viongozi wengine akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi (wa tatu kutoka kushoto) na Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote (katikati).
..............................................................................................
Na. Mwandishi wetu, Dodoma
SERIKALI imeitaka Bodi ya Maziwa na Wadau wote wa maziwa kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha ndani ya miaka miwili ijayo Tanzania inazalisha maziwa ya kutosha ili kusiwe na haja ya kuagiza maziwa nje Nchi.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina leo jijini Dodoma wakati akihitimisha wiki ya Maziwa duniani ambapo ametumia nafasi hiyo kuwataka wenye viwanda vya kusindika maziwa kuongeza uzalishaji zaidi.
Mhe. Mpina amesema kiwango cha kunywa maziwa kwa watanzania kinapaswa kuwa Tani 200 lakini hadi sasa kiwango kinachonyweka ni tani 54 hivyo kuwataka watanzania kuongeza unywaji wa maziwa kwani husaidia kuboresha kinga za mwili na kukuza ubongo
Mhe. Mpina amesema kuwa ili kuhakikisha uzalishaji wa maziwa unaongeza serikali imewaunganisha wawekezaji wa maziwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili waweze kupatiwa mifugo sambamba pia na kutoa msamaha wa kodi kwenye sekta hiyo.
" Ndugu zangu ni muda sasa wa kuhamasisha unywaji wa maziwa nchini kwani Maziwa ni mlo kamili hasa katika kuimarisha mifupa na kuweka ubongo sawa, na yana viini lishe vya kuimarisha pia kinga za mwili”, amesisitiza Mhe. Mpina.
Aidha Mhe. Mpina ameweka wazi kuwa Tanzania ni Nchi ya pili kwa kuwa na Ng'ombe wengi nyuma ya Ethiopia kuwa Tanzania ina Ng'ombe Milioni 33 lakini Ng'ombe wanaozalisha maziwa ni Milioni 1.9 na kiwango cha maziwa kinachozalishwa ni Bilioni tatu ambacho ni kidogo kulinga na mifugo tuliyinayo.
Mhe. Mpina amesema kwa sasa kuna programu ya kuhamasisha unywaji wa maziwa mashuleni kwa baadhi ya mikoa na kusisitiza sasa ni wakati wa kila mkoa kuweka mkakati wa kuhimiza unywaji wa maziwa kwenye kila shule ndani ya mikoa yao.
Pia Mhe. Mpina ametoa wito kwa wawekezaji nchini kutumia fursa ya kuwekeza kwenye usindikaji wa maziwa kwani viwanda vilivyopo kwa sasa vinazalisha asilimia 23 tu ya maziwa na vipo 99.
Mhe. Mpina amehitimisha kwa kuelekeza Halmashauri zote nchini kuzingatia bei elekezi ya chanjo ya mifugo na atakayekaidi hatua kali za kisheria na kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake
Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya Maziwa, Dk Sophia Mrote amesema wiki ya Maziwa imekua ya manufaa sana kwani wiki hii waligawa Lita 1650 kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.
Dkt. Mrote amesema kuwa ndani ya wiki hiyo ya maziwa walikutana wadau wote wa maziwa na kujadili mambo mbalimbali yatakayoweza kuivusha sekta hiyo ili kufikia hatua ya kuzalisha maziwa mengi na kukuza soko hilo hadi nje ya mipaka ya Nchi.
Kind regards Alex Mathias Sonna Chief Editor Fullshangwe Blog Email:alexsonna915@gmail.com Cellphone:+255653257072 Twitter:@ALEXSonna Instagram:@sonnaalex

Magazeti ya Leo Ijumaa June 5 2020


CCM NYAMAGANA YATEMBEA KIFUA MBELE, NI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA KIHISTORIA 260 KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MITANO


Chama Cha Mapinduzi wilayani Nyamagana Cha tembea kifua mbele kwa utekelezaji wa miradi 260 katika kipindi Cha miaka mitano kuanzia Mwaka 2015 Hadi Mwaka 2020 katika uongozi wa serikali ya awamu ya tano ukiongozwa na Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na Mhe. Stanslaus Mabula Mbunge Jimbo la Nyamagana.

Hayo yamebainika katika ziara ya siku nne ya Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Nyamagana ikiongozwa na Mwenyekiti wake Comrade Zebedayo Athuman Wakati wa kukagua miradi 260 ya Maendeleo inayotekelezwa chini ya halmashauri ya Jiji la Mwanza. Ziara hiyo inahusisha ukaguzi wa miradi inayotekelezwa kupitia fedha za Serikali Kuu,  Mapato ya Ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Miradi chini ya Mfuko wa Jimbo pamoja na Miradi kupitia hisani ya Wadau wa Maendeleo katika sekta za elimu, Afya, Miundombinu, Biashara na Uchumi, Maji, Nishati pamoja na Jamii.

Ziara ya siku nne imeanza mnamo Tarehe 03.06.2020 inatarajia kuisha tarehe 07.06.2020. Katika ziara hii Mhe. Zebedayo ameambatana na Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Nyamagana chini ya Mwenyekiti wake DC Dkt. Philis Nyimbi, Ofisi ya Mbunge Jimbo la Nyamagana, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza likiongozwa na Mstahiki Mayor James Bwire pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri Kiamoni Kibamba akiwa na watendaji.

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Nyamagana🇹🇿

CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA SIMIYU KIMETENGA MILIONI 36.7 KUSAIDIA JAMII

Mkuu wa wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga (kushoto) akipokea baiskeli iliyotolewa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu (SIMCU) kwa mtoto Ritha Elias mwenye ulemavu wa miguu(hayupo pichani) kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa SIMCU, Bw. Emmanuel Mwerere makabidhiano hayo yamefanyika sambamba na makabidhiano ya fedha taslimu shilingi 300,000/= Juni 04, 2020 Mjini Bariadi.

Mkuu wa wilaya ya Bariadi Mhe. Festo Kiswaga (kulia) akimkabidhi mtoto Ritha Elias mwenye ulemavu wa miguu fedha taslimu shilingi 300,000/= iliyotolewa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU) kwa ajili ya kumsaidia mtoto huyo katika elimu makabidhiano ambayo yamefanyika sammbamba na makabidhiano ya baiskeli kwa ajili yamtoto huyo Juni 04, 2020 Mjini Bariadi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU) Bw. Emmanuel Mwerere akizungumza kabla ya kukabidhi baiskeli na fedha taslimu shilingi 300,000/= kwa ya kumsaidia mtoto huyo katika elimu, makabidhiano ambayo yamefanyika kati ya Uongozi wa SIMCU na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga Juni 04, 2020 Mjini Bariadi.

Wajumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu(SIMCU) wakiwa katika picha ya pamoja na mtoto Ritha Elias(mbele), viongozi wa Mkoa wa Simiyu, mlezi wa mtoto huyo (kulia) Perpetua Mtaima(kulia) mara baada ya uongozi wa SIMCU kumkabidhi mtoto huyo baiskeli na fedha taslimu shilingi 300,000/= Juni 04, 2020 kwa ajili ya kumsaidia katika elimu.

Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Simiyu, Bw. Ibrahimu Kadudu kabla ya Uongozi wa Chama Kikuu cha ushirika Simiyu(SIMCU) kukabidhi baiskeli na fedha taslimu shilingi 300,000/= kwa ya kumsaidia mtoto huyo katika elimu, makabidhiano ambayo yamefanyika kati ya Uongozi wa SIMCU na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga Juni 04, 2020 Mjini Bariadi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kushoto) na Afisa Elimu watu wazima mkoa wa Simiyu, Mwl. Jusline Gilbert wakiwa katika picha ya pamoja na mtoto Ritha Elias mara baada ya uongozi wa SIMCU kumkabidhi mtoto huyo baiskeli na fedha taslimu shilingi 300,000/= Juni 04, 2020 kwa ajili ya kumsaidia katika elimu. 

***************************** 

Na Stella Kalinga, Simiyu RS 

Chama kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu (SIMCU) kimetenga jumla ya shilingi milioni 36.7 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo elimu na afya katika Mkoa wa Simiyu. 

Hayo yamesemwa na makamu mwenyekiti wa SIMCU, Bw. Emmanuel Mwerere Juni 04, 2020 Mjini Bariadi wakati akikabidhi fedha na baiskeli kwa mtoto Ritha Elias (08) mwenye ulemavu wa miguu. 

“Chama kikuu cha ushirika mkoa wa Simiyu kimetenga jumla ya shilingi 36,700,000/= kati ya hizo shilingi 24,000,000/= itasaidia elimu kwa watoto wenye ulemavu shilingi 12,000,000/= tutanunua mashuka kwa ajili ya Hospitali zote za mkoa wa Simiyu na shilingi 700,000/= kwa ajili ya kumsaidia mtoto Ritha Elias ambaye ni mlemavu wa miguu,”alisema Mwerere. 

“SIMCU leo tunamkabidhi mtoto Ritha Elias kiasi cha shilingi 300,000/= ikiwa ni ada ya shule na nauli ya kwenda na kurudi na baiskeli yenye thamani ya shilingi 400,000/= ambayo itamsaidia akiwa nyumbani na shuleni, “aliongeza Mwerere. 

Aidha, Mwerere ameongeza kuwa mpango huo ni mwendelezo wa shughuli za chama hicho katika kusaidia jamii huku akiongeza kuwa awali walitoa zaidi ya shilingi milioni 3 kwa ajili ya chakula cha wanafunzi waliokuwa kwenye kambi za kitaaluma. 

Katika hatua nyingine Mwerere ameomba makampuni ya pamba yaliyonunua pamba msimu wa wa mwaka 2018/2019 kulipa fedha za ushuru kiasi cha shilingi milioni 729,520,255. 

Awali akiongea kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga ameipongeza SIMCU kwa kutenga fedha hizo na kurudisha shukrani kwa jamii ikiwemo kumsaidia mtoto mwenye ulemavu wa miguu. 

‘’Baadhi ya vyama vya ushirika vinafanya vizuri lakini fedha zao zinaishia kwenye posho na vikao, niwapongeze kwa kutenga kiasi cha milioni 36.7 kwa ajili ya huduma za kijamii ,leo mmekabidhi baiskeli kwa mtoto huyu mwenye ulemavu na mmemwingiza katika mpango wa kumsomesha mpaka mwisho wa masomo yake niwapongeze sana na kingine huyu binti ana kipaji cha kuchora ni mchoraji mzuri sana ’’ alisema Kiswaga. 

Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Simiyu, Ibrahimu Kadudu amesema kurudisha kwa jamii sehemu ya faida ambayo vyama vya ushirika vinapata huo ndio umuhimu wa ushirika, ambapo amebainisha kuwa pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya elimu na afya, awali SIMCU ilichangia fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya janga la CORONA. 

Kwa upande wake bibi wa mtoto wa Ritha Elias, Perpetua Mtaima amesema mtoto huyo alizaliwa akiwa hana miguu yote miwili huku akiongeza kuwa pamoja na ulemavu huo mtoto huyo ana uelewa wa vitu vingi japokuwa ni mdogo na kwa hivi sasa anasoma darasa la tatu katika shule ya watoto wenye ulemavu ya Jeshi la Wokovu iliyopo jijini Dar es salaam na amekuwa akifanya vizuri darasani. 

“Nilikuwa naomba msaada kwa watu mbalimbali akiwemo Mkuu wa wilaya ili mtoto huyu apate elimu na hana miguu nikushukuru sana baba (mkuu wa wilaya ) na mjukuu wangu huyu amekuwa akiniambia siku moja atanibeba kwenye gari lake pia atanipeleka ofisini kwake na akimaliza masomo atapata kazi…nawashukuru wote mlionisaidia kunipatia nauli ya kumpeleka Dar es Salaam’’ alisema Perpetua.