Tuesday, 27 July 2021

UWT Njombe wataka wapinzani kuacha choko choko

 

Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe (UWT) Scolastika Kevela amevitaka baadhi ya vyama vya upinzani kuacha kuleta chokochoko nchini kwa kigezo cha kutaka katiba mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kevela ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameshatolea ufafanuzi suala hilo kwa kusema kuwa apewe muda hivyo wanapaswa kutulia.

Amesema kauli hiyo ya Samia ilipaswa kuheshimiwa na kupokelewa kwa mtazamo chanya na wananchi wote hususani wale wanaoleta chokochoko hasa wapinzani ambao muda mwingi wamekuwa wakianzisha na wakitafuta sababu za kuanzisha chokochoko.

"Rais Samia aachwe afanye kazi yake tuliyomtuma wananchi kwa mujibu wa katiba, ndiyo kwanza uongozi wake una miezi minne madarakani, hizi kelele za wanaotaka katiba zinatolewa kwa lengo la kutaka kumtoa katika reli ya kuwatumikia watanzania." Amesema Scolastika.

Aidha amesema anashangazwa na wapiga kelele hao kuanza kujitokeza kwa wingi na kuleta chokochoko hizo ndani kipindi hilo kifupi cha uongozi wa Rais Samia tofauti na hali ilivyokuwa kabla yake ambapo kulikuwa na kiongozi mwingine katika nafasi hiyo lakini hawakuthubutu kufanya hivyo.

"Mimi kama Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe nalaani chokochoko hizo na zaidi nawaomba watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi hii kuendelea kuunga mkono juhudi anazozifanya Rais wetu kutuletea maendeleo watanzania wote." Amesema Scolastika.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo amempongeza Rais Samia kwa juhudi mbalimbali anazoendelea kuzichukua katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na mataifa mengine duniani

Amesema kitendo cha Rais huyo kukutana na viongozi kutoka mataifa mbalimbali na wakati mwingine kufanya ziara katika mataifa hayo, kunaonyesha dhamira yake ya kushirikiana na mataifa hayo katika masuala mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa uchumi imara wa taifa.

No comments:

Post a Comment