Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi


 Na. Catherine Sungura,Dar es Salaam.

Tanzania imepiga hatua katika kupunguza ugonjwa wa Malaria licha ya baadhi ya mikoa kuwa na maambukizi ya juu ya ugonjwa huo na mikoa ya Arusha,Manyara, Njombe, Kilimanjaro na Iringa kuwa na maambukizi chini ya asilimia moja na mikoa mingine kuwa na maambukizi ya kati.

Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi wakati akifungua kikao kazi cha kwanza cha wataalamu wabobezi wa kudhibiti wadudu wadhurifu waenezao magonjwa tangu kuanzishwa kwa kitengo cha kudhibiti wadudu wadhurifu hapa nchini.

Dkt. Subi amesema kikosi hicho cha wataalum kinaandaa muongozo wa jinsi ya kukabiliana na  wadudu wadhurifu waenezao magonjwa akiwemo mbu.Lengo ikiwa ni kuishauri Wizara njia bora za kukabiliana na wadudu hao.

Alitaja njia hizo ni pamoja na  udhibiti wa mazingira kwa kuhakikisha mbu na wadudu wengine  wadhurifu hawapati sehemu ya kuzaliana na kuweza kusambaza magonjwa na masuala ya usafi  wa mazingira ikiwemo uboreshaji wa nyumba ili kuzuia wadudu wadhurifu  pamoja kuhakikisha watu wanalala kwenye vyandarua vyenye dawa.

Kwa upande wa matumizi ya viuatilifu Dkt. Subi alisema katika kudhibiti mbu alitolea mfano vipo viuatilifu na viuadudu vya kuuwa viluilui kwenye mazalia ya mbu, na amesisitiza kutumia viwanda vya ndani kwa kuwa taasisi taasisi za ndani ambazo zinafanya tafiti na kuonesha mafanikio makubwa ya idadi ya mbu kupungua pamoja mnyororo wa  maambukizi.

“Matumizi sahihi ya vyandarua ni muhimu sana katika kudhibiti Malaria, tunataka angalau zaidi asilimia 80 ya watanzania walalie vyandarua vilivyoweka viuatilifu vya muda mrefu ili kumpunguzia mbu umri wa kuishi na hivyo kupunguza uwezekano wa kusambaza vinmelea vya Malaria ikiwa ni pamoja na upuliziaji wa viuatilifu ukoko ndani ya nyumba”.Alisisitiza Dkt. Subi.

Kwa upande wa ugonjwa wa kichocho Dkt. Subi amesema kikosi hicho kitaangalia pia ni namna gani watadhibiti ugonjwa huo kwenye maeneo yenye majaruba mengi kama mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa mingine, “Mbu wanaeneza pia Matende na Mabusha, Dengue, Chikungunya, Homa ya Manjano na magonjwa mengine yanayokuja kwa vipindi vya mvua kwa hiyo tutapambana kwa kumuangalia mwananchi kudhibiti magonjwa hayo “.

Aliongeza pia wapo Inzi weusi (Simulium) ambao wanaeneza ugonjwa wa Usubi hususan kwenye mikoa ya Mbeya (Tukuyu), Morogoro (Mahenge) na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Iringa hivyo kikosi hicho kitaangalia pia jinsi ya kudhibiti Inzi hao ili kuzuia maambukizi kuliko kuendelea tu kuwamezesha wananchi dawa kila mwaka .

Hata hivyo Dkt. Subi aliwasisitiza wataalam hao kuangalia ni namna gani wanaweza kutumia dawa za asili katika kufukuza mbu  kwa kutumia mbinu za kisasa kwa kumia dawa hizo za asili  katika kufukuza na kua mbu na wadudu wengine wadhurifu waenezao magonjwa.

Share To:

Post A Comment: