Tuesday, 1 December 2020

Mbunge wa Chalinze Akutana na Wananchi wa Kata ya Bwilingu.-Awaahidi kushughulikia Shida kwa Kasi Kubwa

-Atembelea Miradi ya Maendeleo

-Aelekeza kufanywa mchakato wa kuvunjwa Baraza la Ardhi la Kata na kuundwa Tume kuchunguza Malalamiko ya Wananchi kuhusu Huduma Kituo Cha Afya Chalinze.


Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ndg. Ridhiwani Kikwete ameendelea na ziara yake jimboni hapo kwa kutembelea Wananchi wa Kata ya Bwilingu.


Akizungumza katika kueleza nia ya ziara hiyo mh. Mbunge aliwaambia wananchi kuwa dhamira ya ziara hiyo sio kuja kuhutubia bali kwanza ni kuwashukuru wananchi hao kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi kwa kura nyingi zilizomfanya Dr. Magufuli kuibuka mshindi kwa asilimia 94.7 katika Halmashauri hiyo na pili ni kusikia toka kwa Wananchi nini ambayo yamekuwa kero na wangependa wawatume viongozi wao wakayafanyie kazi.


Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Makondomengi, Msolwa Muheshimiwa mbunge aliwahakikishia wananchi juu ya utayari wa serikali ya Awamu ya Tano katika kutatua kero zinqzowakabili ikiwemo ile kubwa ya Ukosefu wa Kivuko kutoka Bomani kwenda Msolwa kinachokwamisha shughuli nyingi ikiwemo hata watoto kwenda shule punde mto unapojaa maji.  Wananchi hao kupitia hotuba walimuahidi Mheshimiwa Mbunge kuwa ujenzi huo utakapo kamilika daraja hilo liitwe kwa jina lake Mbunge jambo ambalo Mh. Mbunge alilikubali lkn akawaomba jina liwe la Mrisho Kikwete kuenzi Boma la kwanza la mtawala lililojengwa huko Makondomengi.


Wananchi hao wa kata ya Bwilingu walishukuru kwa serikali yao kuendelea kulifanyia kazi kero mbalimbali katika maeneo yao ikiwemo barabara, mikopo kwa vikundi vya maendeleo, migogoro ya wakulima na wafugaji.


Wakizungumza wananchi wa Kitongoji cha Bwilingu katika Mkutano wao wa Kitongoji baadae jioni, pamoja na kumshukuru Mbunge na Mheshimiwa Diwani wa Kata hiyo Ndugu Nassar Tamim kwa kuanza vizuri kazi, wameiomba serikali kushughulikia kero za mji wa Bwilingu ikiwemo uhitaji wa barabara za Lami, kuboreshwa kwa huduma za afya kituoni, kero za migogoro ya Ardhi na baraza la ardhi, hitaji la Nishati ya Umeme.


Akizungumza mheshimiwa mbunge aliwahakikishia wananchi wa Bwilingu pia jinsi alimashauri ilivyojipanga kuboresha mazingira ya Usafi na afya kwa mji wa Bwilingu na hasa akiangalia kuwa mji huo ndiyo sura ya halmashauri ya wilaya ya Chalinze. Mh. Mbunge aliwahakikishia wananchi kuwa kero au changamoto mbalimbali walizozitaja zitafanyiwa kazi.


Kuhusiana na kero ya migogoro ya ardhi, mheshimiwa Mbunge alishauri kuangaliwa upya kwa uwezo wa kufanya maamuzi wajumbe wa baraza hilo na kama itawezekana taratibu za uvunjwaji wa Baraza hilo zifanywe ili kutoa haki kwa wananchi wanyonge ambao wanapata  tabu wanapozitafuta haki zao. 


Kwa upande wa afya, Mh. Mbunge ameagiza kuundwa kwa tume kuchunguza malalamiko mbalimbali ya wananchi juu yq kituo cha Afya Chalinze. Akieleza mbele ya Wananchi  Mh.Mbunge alisema,".... Serikali imeleta fedha nyingi, madawa mbalimbali na watumishi ili kuimarisha utendaji na huduma. Kama shida ni wataalamu, upungufu wa madawa ni hatua gani zimechukuliwa hata leo wananchi wanalalamika kuhusu mapungufu hayo. Ndugu Mganga wa Wilaya tunahitaji majibu mara moja ili tujue nini tufanye."


Ziara hiyo itaendelea tarehe 2 Desemba kwa Mbunge kuelekea Kata ya Mkange, kupisha sherehe za Siku ya Ukimwi Duniani ambayo

Kimkoa itafanyika Bagamoyo Tarehe 1 Desemba.

No comments:

Post a comment