Na, Hazla Quire


Wakati walimwengu wakijifungia ndani kwa hofu ya kuambukizwa virusi vya homa kali ya mapafu Corona huku wakipoteza nafasi zao za ajira au hata biashara zao kufilisika,


Hali imekuwa tofauti kwa wafanyabiashara wa tangawizi, mchaichai, malimau, pilipili na ukwaju pale tu vitu hivyo vilipokuwa vinatumika kuongeza kinga na tiba ya kupambana na homa hiyo.


Bw. Emanuel Mollel mfanyabiashara wa tangawizi na ukwaju katika soko la kilombero ameeleza namna janga hilo lilivyo geuka baraka kwa upande wake kwani aliweza kujenga nyumba kwa kipindi hicho.


"Nilikuwa nauza gunia la kilo 160 la tangawizi kwa muda wa siku mbili huku ukwaju nikiwa nauza mpaka kilo 30 kwa siku na kilo moja ni Tsh.3000, hivyo iliniwezesha kujenga nyumba kwa kipindi cha miezi miwili pekee" Alisema Mollel na kuongeza


"Sitaki kukuambia nilikuwa napata kiasi gani kwa siku lakini unaweza kupiga mahesabu mwenyewe, lakini sasa hivi hali imekuwa tofauti kwani unaweza kusota na gunia moja la tangawizi zaidi ya wiki mbili"


Kwa upande wake mfanyabiashara wa malimau Bi. Pendo Akyoo alijivunia kununua pikipiki aliyoikodisha ambayo inamsaidia kukidhi mahitaji yake hasa katika kipindi hiki ambacho biashara hiyo imedorora.


"Biashara ya malimao hivi sasa imeshuka, ukilinganisha na kipindi cha corona, niwaombe watanzania kuendelea kutumia bidhaa hii, kama tuliambiwa yanaongeza kinga ya mwili basi tutambue kuna magonjwa mengi zaidi ya corona na itatusaidia" alibainisha.


Naye Amina Rashid ambaye alipata umaarufu sokoni hapo kwa kuuza mchaichai aliweza kuongeza mtaji wake kutoka Tsh. 20,000 hadi Tsh. 200,000 huku akilimbikiza fedha za kulipa ada kwa watoto wake aliowapeleka shule binafsi.


"Nilifika mahali nauza mchaichai hadi Tsh.50,000 kwa siku fedha ambayo tangu nianze kuuza sijawahi kupata zaidi ya kipindi cha corona na niliweka akiba ya kutosha" alifafanua.


Alidai kutembea porini kutafuta bidhaa hiyo iliyosakwa kama lulu kwa matumizi ya kunywa na kujifukiza lakini hivi sasa haina soko kiasi kwamba inapoteza harufu yake ingali sokoni kwa kukauka.


Hata hivyo licha ya kupata manufaa katika kipindi cha korona lakini wengi wao walisisitiza wananchi kuchukua tahadhari ili janga hilo litokomee kabisa.

Share To:

msumbanews

Post A Comment: