Monday, 16 March 2020

IDARA YA VIJANA KANISA LA WAADVENTISTA WASABATO DODOMA KATI YAJA NA MPANGO WA USAFI WA KUDEKI VYOO SHULE ZA SERIKALI 17 DODOMA ,HUKU WAKISHONA NA KUBRASHI BURE VIATU VYA WANAFUNZI ZAIDI YA 400.

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma

Katika  kuadhimisha juma la Matendo ya Huruma Kanisa la Waadventista Wasabato Ulimwenguni,Idara ya vijana kanisa la Waadventista Wasabato Dodoma kati imeanzisha mpango wa kufanya usafi wa Mazingira  katika shule za  msingi  na sekondari jijini Dodoma  zoezi ambalo limekwenda sambamba na kudeki vyoo ,kushona  pamoja na kubrashi  takriban viatu vya wanafunzi 400  shule ya Sekondari Dodoma .
Akizungumza  na Mtandao huu  Mkurugenzi wa Chama cha vijana watafuta njia [Pathfinder] Kanisa la Waadventista Wasabato Dodoma kati ,Baraka Christopher  Ntalila amesema idara ya vijana kanisani kwa siku ya kwanza imefanya ukarabati  wa miundombinu na usafi vyooni katika shule tatu ambazo ni shule ya sekondari Viwandani,shule ya sekondari Dodoma pamoja na Shule Ya Msingi Makole huku matarajio ni kufikia shule 17 .
Pia amesema wanawatumia vijana wenye talanta mbalimbali kanisani ikiwa ni pamoja na talanta za utengenezaji wa sabuni pamoja wenye talanta za ufundi wa ujenzi huku kanisa nalo likichangia zaidi ya laki tano katika ununuzi wa malighafi ikiwa ni pamoja na Saruji na malighafi za kutengenezea sabuni ya chooni ambapo kila shule wanayoitembelea  wanaacha lita 20 ya sabuni hiyo.
Hata hivyo,Baraka amezungumzia jinsi zoezi la kushona na kubrashi bure viatu vya wanafunzi katika shule ya sekondari Dodoma lilivyokuwa na mwitikio ambapo takribani wanafunzi mia nne [400]wamejitokeza kushonewa na kubrashiwa viatu vyao huku akizungumzia matarajio ya Juma la Matendo ya huruma kwa baadae ni kufanya matendo ya huruma ya kutoa damu,kuwatembelea wafungwa pamoja kuwatembelea watoto yatima.
Monica Mwakaringa na Frida Mbando ni miongoni mwa wanafunzi wanaosoma katika shule ya Sekondari Dodoma  ambapo wao wameelezea kufurahishwa na jambo hilo la pekee ambapo wametoa shukrani kwa Kanisa la Waadventista Wasabato  kwa hatua hiyo ya matendo ya Huruma huku wakiguswa zaidi na zoezi la kushonewa na kubrashiwa viatu bure.
 
Muonekano wa Tundu la choo moja ya shule za serikali jijini Dodoma kabla halijafanyiwa usafi.Muonekano wa tundu la choo baada  ya kufanyiwa usafi.
Mmoja wa vijana wa Chama cha watafuta njia akifanya ukarabati wa sakafu,mlango pamoja na samani za shule Ya Sekondari Viwandani  jijini Dodoma .

Vijana wa Umoja wa Wanafunzi wa Kiadventista Wasabato [ASSA]Shule ya  Sekondari ya Dodoma wakuingana na Chama cha Watafuta njia [Pathfinder]Kanisa la Waadventista Wasabato Dodoma kati katika ushonaji wa viatu.

No comments:

Post a comment