Monday, 2 December 2019

WAHITIMU CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE KAMPASI YA KARUME - ZANZIBAR WATAKIWA KUJIENDELEZA ZAIDI KATIKA ELIMU YAO


Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Stephen Wassira amewataka wahitimu wa Chuo hicho kuhakikisha wanajiendeleza katika Elimu waliyoipata Chuoni hapo kwani Elimu haina mwisho.

Wassira ameyasema hayo wakati wa Mahafali ya 4 ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar ambapo wanafunzi 782 wa kozi mbalimbali wamehitimu masomo yao chuoni hapo na kutunukiwa Astashahada, Stashada na Shahada.

Mwenyekiti huyo ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi wa Mahafalai hayo ya 4 ya kampasi hiyo ameongeza kuwa wahitimu wa Chuo hicho ni wa tofauti sana kwani licha ya kupata Elimu kulingana na kozi zao lakini pia wanapata fursa ya kusoma masuala ya Uongozi, Uzalendo na Maadili.

“ Natoa pongezi  kwa wahitimu waliomaliza katika ngazi mbalimbali za Elimu na pia natumai mtakuwa viongozi bora wa mfano wenye kuonyesha njia na kutatua changamoto na sio watu wa kulalamika kutokana na Elimu nzuri mliyoipata ya Uongozi, Uzalendo na Maadili,”

“ Pia  nendeni mkajitofautishe na wanafunzi wa vyuo vingine kwa matendo kwa kuwa Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kina heshima kubwa kwani kilianzishwa na baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.” Alisistiza mgeni rasmi Wassira.

Amesema katika kuendelea kuboresha Miundombinu ya Chuo hicho, Chuo kinatarajia kujenga hosteli kwa ajili ya wanafunzi ili kutatua changamoto ya makazi na kuwa hosteli hiyo itakapokamilika itapewa jina la Sheikh Thabit Kombo ambaye alikuwa mtu aliyefanya kazi kwa karibu na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ili kuendeleza, kuenzi, na kutunza historia na jitihada za waasisi wa Taifa la Tanzania.

Naye Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila amesema kuwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar kinakua siku hadi siku na hiyo ni kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Chuo na Serikali.Prof. Mwakalika amesema lengo la Chuo ni kuhakikisha kozi zinazotolewa zinaakisi malengo ya Chuo hicho ikiwemo kuhakikisha wanafunzi wanajifunza Uongozi bora, Uzalendo na Maadili hivyo amewaasa wahitimu kuitumia vizuri Elimu waliyoipata ili kujisaidia wenyewe pamoja na jamii inayowazunguka.

“Chuo hiki kinaenzi mambo mengi yaliyofanywa na Mwalimu nyerere  na hasa katika masuala ya Uongozi bora kama Mwalimu alivyosema kuwa Maendeleo ya kweli yanahitaji Watu, Ardhi, Siasa safi na Uongozi bora.”Alisisitiza Prof. Mwakalila.Imetolewa na Kitengo cha Uhusiano

Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere

2/12/2019

No comments:

Post a comment